Kontena 700 zilizokwepa ushuru kaa la moto serikalini

04Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kontena 700 zilizokwepa ushuru kaa la moto serikalini

KONTENA 700 zinazodaiwa kuingizwa nchini bila kulipiwa kodi, zimekuwa kama kaa la moto kutokana na mamlaka mbalimbali za serikali kujiweka kando kuliweka wazi.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo

Kila mamlaka ilipoulizwa na Nipashe kuombwa ufafanuzi kuhusiana na kontena hizo zinazodaiwa kuingizwa na kiongozi mwandamizi nchini haikuwa tayari kutoa maelezo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imesema madai yaliyoibuliwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, kuhusu kiongozi huyo mkubwa nchini kukwepa kodi baada ya kuingiza mzigo wa kontena hizo bandarini wao hawawezi kuyazungumzia.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo, alipoulizwa jana na Nipashe kwa njia ya simu kuhusu kontena hizo, alisema mamlaka haiwezi kuyazungumzia kwa sababu yawezekana ni taarifa za ndani.

“Yawezekana hizi ni taarifa za ndani ndiyo maana Polepole hakutaja jina wala kampuni husika. Kwa sasa hatuwezi kuzungumzia chochote kuhusu hizo kontena na sisi tumeona taarifa kwenye gazeti,” alisema.

Juzi, Nipashe ilichapisha habari ambayo Polepole Jumamosi iliyopita akiwa kwenye kongamano la umuhimu wa amani na mapambano dhidi ya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu, alisema kiongozi huyo (jina hakulitaja) alikuwa na kontena 700 bandarini amekwepa kodi.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Polepole alisema “Yupo kiongozi mmoja mkubwa sana Tanzania sitamsema hata Takukuru wanamfahamu, ila mniwie radhi sitamtaja jina, alikuwa na kontena 700 bandarini amekwepa kodi.

“Kila kontena moja lilikuwa na futi 40, huyu kiongozi alitaka Rais amsaidie, lakini Rais Magufuli alimwambia lipa kodi uende zako. Huyu kiongozi mpaka sasa amenuna,” alidai.

“Hivi ninavyoonea mpaka sasa amenuna. Rais Magufuli kazi yake ni kushughulika na watu walionuna. Siku zote ukisimamia haki hupendwi. Mtume alisimamia haki hakupendwa, Yesu alisimamia haki Wayahudi wakamuua, Ayubu alisimamia akapoteza kila kitu hadi familia yake.”

Polepole alidai hakuna mtu anayesimamia haki ambaye ameishi maisha ya starehe bali huishi kwa imani.

Kongamano hilo liliandaliwa na Jumuiya ya Waislamu wa Shia Tanzania na kuhudhuriwa na viongozi wa vyama vya siasa, chama tawala na vyama vya upinzani, viongozi wa dini na wadau wengine.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo la kontena 700 kama wizara yake inafahamu alisema ndio kwanza analisikia kutoka kwa mwandishi na kuomba aulizwe Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango ili kujua ni la kweli au la na kama alilipa kodi.

Gazeti hili lilimtafuta Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango ambaye pia ni Msemaji wa wizara hiyo, Benny Mwaipaja, ambaye alisema suala hilo halipo wizarani hapo.

“Suala hili halipo wizarani, ni la TRA labda ujaribu huko kutafuta majibu,” alisema.

Habari Kubwa