Mo Dewji moto Simba, hapoi

04Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mo Dewji moto Simba, hapoi

HUKU mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wakirejea mazoezini kesho kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Mtibwa Sugar itakayopigwa Uwanja wa Uhuru Septemba 17, mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo-

-Mohamed "Mo" Dewiji ameendelea kuwasha moto wa kurejesha morali kwa wachezaji na mashabiki wa timu hiyo.

Mashabiki wa Simba wamekatishwa tamaa na klabu yao baada ya kutolewa raundi ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa faida ya bao la ugenini na UD Songo ya Msumbiji kufuatia kutoka suluhu ugenini kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Na mwishoni mwa wiki Mo aliwataka Wanasimba kumsamehe kwa kuwa mkimya na maumivu ya matokeo waliyoyapata, ambapo aliwataka kutovunjika moyo wala kukata tamaa.

Lakini jana Mo alifunguka tena akiwaamsha mashabiki na wachezaji wa klabu hiyo kwa kueleza: "Ujumbe huu ni kwa wachezaji wa @Simba SC Tanzania na mashabiki, mabingwa hawaelezwi kwa ushindi wao bali namna wanavyoanza baada ya kuanguka."

 Kocha wa Simba, Patrick Aussems, alitoa mapumziko ya siku mbili kwa wachezaji wake juzi, hivyo kesho watarejea tena mazoezini katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Mtibwa wakati huu ambao ameweka wazi kuwa baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa wanataka kuvuna mataji yote ya ndani msimu huu, la Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka nchini (FA Cup).

Habari Kubwa