Hospitali yanunua CT-Scan ya kisasa

05Sep 2019
Cynthia Mwilolezi
MBULU
Nipashe
Hospitali yanunua CT-Scan ya kisasa

HOSPITALI ya Rufani ya Kilutheri ya Haydom wilayani Mbulu mkoani Manyara, inayohudumia zaidi ya wagonjwa 120,000 kwa mwaka, imenunua mashine mpya ya kisasa ya uchunguzi ya mionzi (CT-Scan) ambayo kwa miaka miwili hakukuwa na huduma hiyo baada ya iliyokuwapo kuharibika.

ct-scan machine

Hospitali hiyo kwa mwaka huhudumia wastani wa wagonjwa 105,296 wa nje na 14,020 wa ndani wa mikoa ya Manyara, Arusha, Tabora, Singida, Dodoma na Simiyu.

Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk. Emmanuel Nuwass, akizungumza na waandishi wa habari juzi, alisema Sh. milioni 800 zimetumika kuinunua mashine hiyo nchini Ujerumani na kuisafirisha hadi hospitalini hapo.

Dk. Nuwass alisema awali mashine iliyokuwapo iliharibika miaka miwili iliyopita, hivyo kusababisha wagonjwa wengi kukosa huduma ya vipimo hivyo.

Alisema kutokana na ukosefu wa mashine hiyo, iliwabidi watu wa eneo hilo kufuata vipimo takribani kilomita 400 hadi 600 kwenye hospitali za kanda za KCMC Kilimanjaro na Bugando Mwanza.

Alisema mashine hiyo ya kisasa itasaidia wagonjwa wengi hasa wasio na kipato kupata vipimo kwenye eneo la karibu na wanatarajia itazinduliwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, hivi karibuni.

Catherine Faustine, mkazi wa eneo hilo, alisema wananchi wengi wameshindwa kupata huduma hiyo kutokana na umbali mrefu wa kufuata katika hospitali zingine kubwa.

"Kuna baadhi ya watu walifariki (dunia) kwa sababu hawana fedha za kwenda kupimwa katika hospitali za mbali kama KCMC Moshi au Muhimbili, Dar es Salaam. Tunashukuru kwa kupata mashine hii," alisema.

Mtaalamu wa Mionzi wa Hospitali hiyo, Paulo Fissoo, alisema mashine hiyo ina uwezo mkubwa zaidi tofauti na ile ya awali iliyoharibika.

Hospitali ya Haydom inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu,  ilianzishwa na wamisionari wa Norway mwaka 1955 ikiwa na vitanda 50 na sasa ina vitanda 420.

Wagonjwa wanaopata huduma hospitali hiyo wanatoka wilaya za Mbulu, Hanang na Babati mkoani Manyara, Karatu mkoani Arusha, Igunga mkoani Tabora, Iramba na Mkalama mkoani Singida, Kondoa mkoani Dodoma na Meatu mkoani Simiyu.

Habari Kubwa