Bil. 4.1/- kutumika kujenga barabara

05Sep 2019
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe
Bil. 4.1/- kutumika kujenga barabara

HALMASHAURI ya Jiji la Arusha imekabidhi mradi wa Sh. bilioni 4.1 wa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kampuni ya ujenzi ya Sinohydro Corporation Ltd , unaotarajiwa kuanza Septemba 11, mwaka huu.

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sifael Kulanga

Barabara hiyo ni nyongeza ya mkataba na itajengwa kutoka Kisongo hadi Bypass na itakuwa na urefu wa kilometa 3.44 kupitia fedha za mradi wa Miji Mkakati ya Tanzania (TSCP ), inayoratibiwa na Benki ya Dunia chini ya Ofisi ya Rais (Tamisemi).

Akizungumza baada ya kuukabidhi mradi kwa kampuni hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Sifael Kulanga ambaye ni mwanasheria wa jiji hilo, alisema mradi huo ni wa nyongeza na utatekelewa ndani ya miezi minne hadi Januari 11, mwakani.

Alisema mradi huo utasaida kuondoa msongamano wa magari katikati ya Jiji la Arusha na una manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na utasaidia usalama kwenye uwanja mdogo wa ndege badala ya kukata katikati ya uwanja na barabara hiyo itasaidia kuchepuka pembezoni mwa uwanja.

"Barabara hii ina umuhimu mkubwa sana katika uwanja wetu wa ndege na maeneo ya shule ya sekondari na itafungua fursa kwa wanaowahi katikati ya jiji kutoka stendi kubwa ya mabasi ya mkoani inayotarajiwa kujengwa Olasit."

Mhandisi wa Barabara wa Kampuni ya Snohydro, Lang Yang Shang, alisema wataifanya kazi hiyo ndani ya muda uliopangwa mkataba na kwa viwango vilivyowekwa na kwa ubora.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mhandisi Augusti Mbuya, alisema barabara hiyo, ni muunganiko wa bypass na itarahisisha mchepuko na kusaidia usalama, na aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutenga fedha hizo.

Alisema mradi huo utaanza Septemba 11, mwaka huu na jana ilikuwa kuweka makabidhiano kwa Jiji kumkabidhi rasmi mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.

Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema barabara hiyo ni sehemu ya mkataba uliotiwa saini wiki iliyopita na utakuwa kielelezo cha kueleza jinsi utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kwa wananchi mwaka ujao jinsi serikali ilivyotekeleza miradi yake.

Habari Kubwa