Kiongozi mbio za Mwenge atema cheche

05Sep 2019
Nebart Msokwa
CHUNYA
Nipashe
Kiongozi mbio za Mwenge atema cheche

SERIKALI wilayani Chunya katika Mkoa wa Mbeya, imeagizwa kuhakikisha inakamilisha marekebisho ya miradi miwili ambayo Mwenge wa Uhuru umezindua na kukabidhi taarifa kabla haujatoka katika mkoa huo.

Agizo hilo lilitolewa jana asubuhi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Mzee Ali, wakati wa makabidhiano ya Mwenge huo kati ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi, na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika.

Kiongozi huyo aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na kukamilisha vyoo kwenye nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Kambikatoto ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua familia mbili na kupaka rangi ya pili ili iendelee kutumika.

Mradi mwingine alioutaja Ali ni zahanati ya Isangawana ambayo aliagiza shimo la kuchomea taka liongezwe kuchimbwa kwa madai kuwa lililochimbwa ni fupi na likibaki kama lilivyo, baadhi ya taka zitakuwa zinashindwa kuungua.

Pia katika zahanati hiyo, alisema baadhi ya maeneo swichi za umeme hazijawekwa, hivyo zinatakiwa kuwekwa haraka kabla umeme haujaingizwa.

"Nawashukuru sana viongozi wa Wilaya ya Chunya kwa kusimamia vizuri miradi ambayo tumeizindua na tuliyoiwekea mawe ya msingi. Sasa hakikishani ile miradi iliyoonekana kuwa na upungufu mnaikamilisha na kutukabidhi taarifa kabla hatujahama Mbeya," alisema Ali.

Aidha, aliwashukuru viongozi wa wilaya hiyo kwa kusimamia vizuri miradi kwa madai kuwa mingi imetekelezwa kwa viwango vinavyostahili tofauti na maeneo mengine ambayo alidai wamekuwa wakiikataa baadhi ya miradi kutokana na kutekelezwa chini ya kiwango.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Chunya ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Mahundi, alishukuru kwa Mwenge huo kumaliza salama mbio katika wilaya yake kabla ya kukabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya.

Alisema atahakikisha anashirikiana na viongozi wengine wa wilaya hiyo kusimamia na kuhakikisha miradi iliyotajwa kuwa na mapungufu inarekebishwa mapema kama walivyoelekezwa na kukabidhi taarifa ya utekelezaji mapema.

Mahundi aliwashukuru viongozi wa mbio za Mwenge kwa ushauri walioutoa kwa wilaya yake na kwamba watahakikisha wanazingatia ushauri huo na kuufanyia kazi ili miradi yote inayotekelezwa inakuwa na viwango vinavyoainishwa.

"Tunashukuru kwa maelekezo na tutahakikisha tunayatekeleza kabla ya muda tuliyopewa, lakini tunawashukuru viongozi hawa kwa kutupatia changamoto maana tunaamini zitatusaidia katika kutekeleza miradi yote," alisema Mahundi.

Mwenge wa Uhuru uliingia katika wilayani Chunya ukitokea katika Mkoa wa Tabora, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alikabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri, katika Kata ya Kambikatoto.

Chalamila alisema miradi itakayowekwa mawe ya msingi na itakayozinduliwa ndani ya mkoa wake ni 59.

Habari Kubwa