Wapania kuongeza uzalishaji maharage

05Sep 2019
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Wapania kuongeza uzalishaji maharage

KIKUNDI cha wanawake wanaolima maharage kwenye Kata ya Mshewe wilayani  Mbeya kijulikanacho kwa jina la 'Zinduka' kimesema kinakusudia kuongeza uzalishaji wa zao hilo baada ya kupewa mtambo wa kisasa wa kukaushia maharage.

maharage

Kikundi hicho kilikabidhiwa mtambo wa kisasa wa kukaushia zao hilo unaotumia nishati ya jua (bean solar drier) na taasisi ya kimataifa inayoshughulikia kilimo cha mazao ya kitropiki (CIAT) ili kukisaidia kikundi hicho kuokoa mazao yaliyokuwa yanaoza kutokana na kushindwa kukauka hasa kipindi cha mvua.

Wakizungumza na Nipashe jana, wanachama wa kikundi hicho walisema kabla ya kupewa mtambo huo walikuwa wanapata shida kukausha maharage kipindi cha mvua na kusababisha sehemu kubwa ya mavuno kupotea kwa kuoza.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Witness Sikayange, alisema kikundi hicho kina wanachama 21 na kinalima ekari 300 za maharage na kwamba kwa mwaka wanalima misimu mitatu ukiwamo mmoja wa kiangazi ambao wanatumia mbinu ya umwagiliaji.

Alisema mavuno mengi wanapata msimu wa mvua, hivyo kusababisha mazao kuoza yakiwa shambani au yakiwa yamevunwa na kuhifadhiwa ndani ya nyumba na hatimaye kukosa soko hali ambayo imekuwa ikiwasababishia hasara.

"Tunawashukuru CIAT kwa mtambo huu na tunaamini kuwa utatuongezea nguvu ya kuzalisha, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo tulikuwa tumeanza kupunguza uzalishaji. Hawa wataalamu wametueleza kuwa mtambo huu una uwezo mkubwa wa kukausha mazao," alisema Sikayange.

Alisema kikundi hicho kimekuwa kikishirikiana na wataalamu wa kilimo kutoka katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi ikiwamo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) Kituo cha Uyole, wataalamu kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Ofisa Kilimo wa Kata hiyo.

Alisema kabla hawajaanza kushirikiana na wataalamu hao walikuwa wanatumia mbegu za kienyeji pamoja na mbinu duni za kilimo hali iliyokuwa inawafanya wazalishe chini ya kiwango, lakini kwa sasa wanazalisha kuanzia kilo 600 mpaka 800 kwa ekari.

Mratibu wa Mtandao wa Utafiti wa Maharage Kusini mwa Bara la Afrika, Rolland Chirwa, alisema mtambo huo una uwezo wa kukausha tani moja ya maharage kwa siku na kwamba ni salama kwa mazao kutokana na kuzuia mifugo kula na mvua kunyeshea.

Alisema waliamua kukisaidia kikundi hicho cha Zinduka baada ya kubaini kuwa kina uwezo mzuri wa kuzalisha na kina watu wanaojituma ikilinganishwa na vikundi vingine.

Chirwa alisema kwa kawaida mazao ambayo yameoza hayawezi kuuzika sehemu yoyote na badala yake inakuwa hasara kwa wakulima na akawataka wanakikundi hao kuutunza vizuri ili wafaidike zaidi.

Mtafiti wa Maharage kutoka Tari Uyole, Agness Ndunguru, alisema moja ya vitu walivyokisaidia kikundi hicho ni pamoja na kuwapatia elimu ya kilimo bora na kuwasaidia mbegu za kisasa.

Habari Kubwa