Katibu Mkuu ampa kibarua kizito DMO

05Sep 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Katibu Mkuu ampa kibarua kizito DMO

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk. Dorothy Gwajima, amemwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya Chamwino, kuifanyia kazi haraka changamoto ya ukosefu wa kitanda cha kujifungulia wajawazito katika zahanati ya kijiji cha Chiboli wilayani humo.

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk. Dorothy Gwajima

Dk. Gwajima alitoa agizo hilo jana alipoitembelea zahanati hiyo na kukagua miundombinu mbalimbali.

"Suala la ukosefu wa kitanda kwa ajili ya wajawazito namtaka mganga mkuu wa wilaya kuifanyia kazi ndani ya siku tatu kiwe tayari kimeshafika hapa ili kinamama hawa waendelee kupata huduma kama kawaida," alisema Dk. Gwajima.

"Kitanda hicho anatakiwa kukileta haraka ndani ya siku tatu, kitatoka wapi yeye atajua kwani MSD wapo hapa Dodoma. Anatakiwa kukileta haraka na nitampigia simu," aliongeza Dk. Gwajima.

Awali, muuguzi wa zahanati hiyo, Shija Makeja, alimweleza naibu katibu mkuu huyo kuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa watumishi.

"Mmoja wa watumishi wetu alifariki (dunia) hivi karibu, hivyo tumebaki watumishi wawili tu. Tunaomba serikali kama inaweza kutuongezea wengine ili kuongeza nguvu," alisema Makeja.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ernest Mgora, alimwomba Naibu Katibu Mkuu  kuwawezesha kujenga kituo cha afya kwa kuwa hivi sasa zahanati hiyo inazidiwa na idadi ya wagonjwa.

"Tunaiomba serikali kama inawezekana tujenge kituo cha afya kwani hii zahanati yetu inatumika na watu kutoka katika vijiji vingine vitatu hata vile vya mkoa jirani wa Iringa kuja hapa kupata tiba," alisema Mgora.