Magari mabovu barabarani kukamatwa

05Sep 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Magari mabovu barabarani kukamatwa

SERIKALI imeagiza kuanzia Oktoba Mosi, mwaka huu, kukamatwa magari yote mabovu yanayotembea yakiwamo yale ambayo hayajakaguliwa na kupewa stika ya usalama barabarani na Jeshi la Polisi.

Magari mabovu barabarani

Uamuzi huo umefanywa baada ya kikao cha siku mbili cha Baraza la Usalama Barabarani kilichofanyika jijini hapa na kubaini chanzo cha ajali kubwa ambazo huleta hisia kali kwa jamii ni magari mabovu ambayo hutembea barabarani ovyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kikao hicho kilichojumuisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na mamlaka husika, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, alisema katika baraza hilo kuna kamati ndogo ambazo zimepewa jukumu la kufanya uchunguzi wa ajali ambazo zimetokea hivi karibuni na kuwasilisha ripoti za uchunguzi.

Alisema moja ya kamati zilizoteuliwa ni ile ya ajali na usafirishaji ambayo itaendelea kufanya uchunguzi wa kina na baadaye kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuzuia ajali ikiwa ni moja ya malengo waliojiwekea ya kupunguza ajali zinazotokea barabarani.

"Tumegundua ajali kubwa husababishwa na na magari mabovu, hivyo tumejipanga kuyaondoa magari hayo kuanzia Oktoba Mosi," alisema Masauni.

Kutokana na hali hiyo, alisema inaonyesha jinsi gani mwaka huu ukaguzi wa magari mabovu haujafanyika ipasavyo, hivyo jitihada zaidi zinaendelea katika udhibiti wa magari mabovu kuendelea kuwapo barabarani.

Alisema hiyo ni moja ya mikakati ya muda mrefu ambayo serikali imejiwekea kwa kushirikiana na mamlaka zingine lengo likiwa kuona ajali za barabarani zinazosababishwa na uzembe zinatoweka kabisa.

Katika kutekeleza hilo, alisema jamii inapaswa kuzingatia agizo hilo ili ifikapo  Oktoba Mosi, magari yote mabovu ambayo hayajafanyiwa ukaguzi na kupewa stika ya usalama barabarani, yaondolewe barabarani.

"Naomba jamii izingatie agizo hili hakuna msamaha wowote utakaotolewa ukibainika na makosa hayo," alisema Masauni.

Masauni pia alisema moja ya mikakati waliyojiwekea ni kuhakikisha usimamizi na udhibiti wa magari mabovu unafanyika kiufasaha.

Sambamba na hilo, alisema serikali kupitia mpango mikakati iliyojiwekea imepanga kuweka askari katika vituo maalumu ili kupunguza kusimamishwa kwa magari ovyo barabarani hususani yale yanayokwenda masafa ya mbali.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni pamoja kutaka kuleta ufanisi katika utendaji kazi kwenye magari hayo hususani mabasi, maroli pamoja na mengine yanayokwenda masafa marefu.

Habari Kubwa