Wizara yalalamika ukataji barabara kupitisha mabomba

05Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Wizara yalalamika ukataji barabara kupitisha mabomba

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe, amesema changamoto kubwa inayoikabili wizara hiyo ni baadhi ya taasisi kukata barabara kwa ajili ya kupitisha huduma za kijamii hali inayoleta uharibifu mkubwa wa barabara.

Aliyasema hayo Ikulu mjini Zanzibar wakati wizara hiyo ikiwasilisha taarifa za Utekelezaji wa Mpango Kazi wa Wizara hiyo kwa mwaka 2018/2019.

Alisema kumekuwapo na ukataji ovyo wa barabara na kupitisha huduma za maji na umeme unaofanywa na taasisi bila kuzingatia gharama za utengenezaji wa barabara hizo.

"Kuna baadhi ya taasisi mbili kwa nyakati tofauti hukata barabara kila mmoja na kupitisha miundombinu, jambo ambalo kama kungekuwapo na ushirikiano kwa taasisi kukaa pamoja kabla ya ujenzi na kupitisha miundombinu yao katika eneo moja, kusingekuwa na uharibifu huu wa barabara," alisema.

Naye Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Sira Ubwa Mamboya, alisema katika kipindi hicho wizara imepata mafanikio makubwa, ikiwamo kukamilisha ujenzi wa kilomita 28 za barabara mbalimbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha lami.

Alisema wizara inaendelea na ujenzi wa Barabara ya Bububu–Mahonda–Mkokotoni, yenye urefu wa kilomita 31, wakati kilomita 28.8 za barabara hiyo zikiwa tayari zimewekwa kifusi tabaka la mwisho, pamoja na kuweka lami ya maji kilomita 14 katika upande mmoja wa barabara.

Akigusia azma ya serikali katika kuimarisha ujenzi wa miundombinu, Dk. Sira alisema wizara imefanikiwa kununua vifaa vya ujenzi ambavyo tayari vimewasili nchini.

Alisema wizara imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa meli mpya ya mafuta (MT Ukombozi 11), ambayo imeshawasili nchini tangu Agosti 7, mwaka huu.

Dk. Sira alisema wizara kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege imefanikiwa kuimarisha huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) kwa kuimarisha ulinzi na usalama, ufungaji wa mkanda wa mizigo, ununuzi wa mashine tano mpya za ukaguzi, kuimarisha ukumbi wa marais pamoja na kuendelea na ufungaji wa vipoza hewa.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, alisema kuna umuhimu kwa wizara na taasisi za serikali kushirikiana ili kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wakati.

Alisema kuna baadhi ya miradi ya maendeleo ambayo imeshindwa kutekelezwa kwa wakati, kutokana na ukosefu wa ushirikiano, baada ya taasisi kuwa na mitizamo inayokinzana katika suala la uwekaji wa miundombinu.

Alieleza kuwa, kabla ya mradi wowote wa maendeleo kuanza kutekelezwa, ni muhimu kwa taasisi zenye miundombinu inayoingiliana kukaa pamoja na kuangalia itakavyowekwa ili kuepuka gharama na uharibifu usio wa lazima.

Alisema kuna baadhi ya barabara zilizokatwa kwa ajili ya kupitisha miundombinu bila ya wenye mamlaka kuarifiwa hivyo alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ustaarabu wa kufanyakazi kwa pamoja ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazojitokeza.

Dk. Shein alitoa ufafanuzi huo baada ya uongozi wa wizara hiyo kuelezea changamoto kubwa ya uharibifu wa barabara unaotokana na baadhi ya taasisi kupitisha miundombinu, ikiwamo ya maji na taa.

Habari Kubwa