Wanawake washauriwa kutooneana wivu nafasi za uongozi

05Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Wanawake washauriwa kutooneana wivu nafasi za uongozi

NAIBU Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mgeni Hassan Juma, amewataka wanawake kuwa na uthubutu wa kugombea nafasi mbalimbali za uamuzi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Aliyasema hayo katika mkutano wa kuhamasisha jamii kuhusu nafasi za uongozi kwa wanawake ulioandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), uliofanyika Shehia ya Magomeni, Mjini Unguja.

Alisema bado uthubutu wa wanawake ni mdogo na ndio maana katika vyombo vya kutunga sheria kumekuwa na ushiriki mdogo wa wanawake ikilinganishwa na wanaume.

Aliwataka wanawake hao kubadili tabia ya kuoneana wivu na roho mbaya wanapogombea nafasi za uongozi majimboni na badala yake kuwapa ushirikiano.

Pia aliwataka kupaza sauti zao katika vyama vyao vya siasa ili kuondoa changamoto zinazowakabili wanapogombea nafasi za uongozi ikiwamo rushwa.

Wakizungumza katika mkutano huo wanawake wa Shehia ya Magomeni, walisema elimu duni waliyonayo wanawake wanashindwa kupata nafasi za uongozi.

"Tokea nyuma wanawake tumenyimwa elimu na wazazi wetu walikuwa wakiwapa elimu zaidi watoto wa kiume na ndio maana wanawake tupo nyuma,” alisema Tatu Othman Kipingu, mkazi wa Shehia hiyo.

Alisema changamoto nyingine inayowakwaza wanawake ni kipato kidogo walichonacho na kushindwa kumudu gharama za uchaguzi.

Naye Khuzaima Hamdani, aliiomba serikali kupitia Tume ya Uchaguzi kupunguza gharama za uchukuaji wa fomu hasa kwa wanawake kwa kuwa kiwango kilichowekwa ni kikubwa.

"Tunaiomba serikali ipunguze gharama za uchukuaji wa fomu ili na sisi wanawake tupate fursa ya kugombea nafasi za uongozi,” alisema.

Alisema ushindani mkali wa vyama vya siasa umesababisha wanawake kutopata nafasi za uongozi kwa sababu baadhi ya vyama vinaona vikimsimamisha mwanamke vitakosa nafasi.

Hata hivyo, alisema vikwazo vingine vinavyowakabili wanawake ni rushwa ya fedha na ngono kwa kuwa wanapogombea nafasi za uongozi hudaiwa rushwa hiyo.

Habari Kubwa