Wimbo wa Msechu roho ya Jamafest 2019

05Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wimbo wa Msechu roho ya Jamafest 2019

WIMBO mpya wa Jamafest 2019 ulioimbwa na msanii Peter Msechu, umeteuliwa kuwa wimbo maalum katika Tamasha la Utamaduni la Afrika Mashariki linalotarajiwa kufanyika nchini kuanzia Septemba 21-28, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Peter Msechu

Taarifa za wimbo wa Jamafest 2019 kuteuliwa kuwa wimbo rasmi wa tamasha hilo maarufu Afrika Mashariki zilifahamika baada ya Msechu kuandika katika ukurasa wake wa Instagram akimshukuru Mungu kwa wimbo wake huo kupitishwa.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoa ufafanuzi juu ya kuchaguliwa kwa wimbo huo kuwa maalum katika tamasha la Jamafest, Msechu alisema alituunga baada ya uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwaomba wasanii mbalimbali kutunga wimbo ambao ungetumika kama wimbo maalum wa tamasha.

“Wasanii tupo wengi sana kwa mimi kupata fursa hii ya kuimba katika ufunguzi wa tamasha hili kubwa la Jamafest kwangu ni heshima kubwa sana. Tulikuwa wasanii wengi tuliotunga nyimbo kwa ajili ya tamasha, lakini wimbo wangu umechaguliwa ni furaha kubwa,” alieleza Msechu.

Alisema kwa sasa anaandaa video ya wimbo huo ili uweze kutumika kuhamasisha Watanzania na watu wa Afrika Mashariki kushiriki katika tamasha ambalo lina lengo la kudumisha urithi wa utamaduni, sanaa za mikono na ubunifu.

Akizungumzia wimbo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Tamasha la JAMAFEST, Joyce Fissoo, alisema mchakato wa uteuzi wa wimbo rasmi kwa ajili ya tamasha hilo haukuwa rahisi kwani kulikuwa na ushindani mkubwa  kutokana na wasanii wengi kujitokeza na kufanya utunzi wa wimbo.

“Mchakato wa kupata wimbo wa tamasha ulikuwa mgumu kutokana na wasanii kujitokeza na baada ya kusikiliza nyimbo zote ndipo sekretarieti ya maandalizi ya tamasha inayoundwa na wajumbe kutoka nchi sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikauchagua wimbo wa Jamafest 2019 ulioimbwa na Msechu kuwa ndio wimbo wa tamasha,” alieleza Fissoo.

Tamasha la Jamafest ni tamasha lililopitishwa na Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuenzi na kulinda utamaduni wa makabila ya Afrika Mashariki. Tamasha hili hufanyika kila baada ya miaka miwili katika nchi wanachama ambapo mwaka huu litafanyika nchini kuanzia Septemba 21-28 katika Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa