Kiungo Mtanzania atamani kutua EPL

05Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kiungo Mtanzania atamani kutua EPL

KIUNGO mshambuliaji wa Minnesota United ya Marekani, Mtanzania Ally Ng’anzi, amesema anamshukuru Mungu kupata nafasi katika klabu hiyo, lakini ndoto yake kubwa ni kuona anasajiliwa na klabu mojawapo inayoshiriki Ligi Kuu England.

Akizungumza na gazeti hili jana, Ng'anzi, alisema kila siku amekuwa akipambana kufanya vema katika timu yake kuanzia mazoezini, hadi kwenye michezo ya ligi, kwa sababu anataka kuona anafanikiwa kuwashawishi mawakala wanaofuatilia ligi hiyo.

Ng'anzi alisema anaamini mchezaji yeyote ambaye anajituma, kufikia mafanikio ni jambo la kawaida na si miujiza.

"Naendelea vizuri katika timu yangu, ninafanya mambo makubwa kila ninapopata nafasi ya kucheza, kwa sababu ninataka kutimiza ndoto yangu ya kwenda kucheza Ligi Kuu ya England, bado sijafika mwisho," alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Singida United ya mkoani Singida.

Aliwataka pia wachezaji wengine chipukizi wa Tanzania wanaopata nafasi ya kwenda kufanya majaribio katika klabu za Ulaya kuhakikisha wanapeperusha vema bendera ya nchi.

Baada ya kufanya vema huko Marekani, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Vijana wa umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Zuberi Katwila, amemjumuisha nyota hiyo katika kikosi chake ambacho baadaye mwezi huu kitakwenda kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati yatakayochezwa jijini Kampala, Uganda.

Habari Kubwa