Kuachiwa ndege ATCL kwaibua furaha, gumzo

05Sep 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kuachiwa ndege ATCL kwaibua furaha, gumzo

MUDA mfupi baada ya ndege aina ya Airbus A220-300 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Afrika Kusini kuachiwa, imeibuka furaha na gumzo kutoka kwa viongozi mbalimbali wa serikali.

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini humo,  alisema  mlalamikaji hakutarajia kuwa Tanzania itashinda kwenye kesi ya kuzuiwa kwa  ndege hiyo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na mkulima Hermanus Steyne katika Mahakama Kuu ya Gauteng, nchini humo, kwa alichodai anaidai serikali ya Tanzania Sh. milioni 373 baada ya mali zake kutaifishwa na serikali ya awamu ya kwanza Januari 1982.

Ndege hiyo ilishikiliwa Agosti 23, mwaka huu, baada ya kwenda nchini humo kwa safari za kawaida, kutokana na kuanzishwa kwa njia mpya ya safari za ndege za ATCL nchini humo.

Akizungumza na televisheni ya taifa jana kwa njia ya simu, Kaimu Balozi wa Tanzania nchini humo, Richard Lupembe, alisema ndani ya mahakama hiyo ilikuwa ni furaha kubwa kwa kuwa awali hawakuwa na matarajio ya kushinda kwa kuwa waliofungua kesi walikuwa na matarajio ya ushindi na ndiyo maana wamekata rufani.

“Lakini baada ya Jaji kusema tumeshinda sisi na wao wameshindwa, kila mtu akaingia mlango wake anaoujua yeye, sisi tukabaki na furaha yetu na kuanza kujipanga kuelekea uwanja wa ndege,” alisema.

Kuhusu kukata rufani, alisema walioshindwa wanajitahidi kukata rufani, lakini hakuzuii ndege hiyo kuondoka nchini humo na kufanyakazi kama kawaida.

“Wamekata rufani kwenye Mahakama ambayo imesikiliza shauri la awali,” alisema Balozi Lupembe.

“Baada ya hukumu ya Jaji hawakutakiwa kujibu lolote zaidi ya kusikia hukumu…alitushtaki anatudai, lakini baada ya kujitetea imeonekana hatudai chochote na tumeruhusiwa ndege yetu kuondoka.”

WAZIRI WA UJENZI

Jijini Dar es Salaam  Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alithibitisha kuachiwa kwa ndege hiyo na kueleza kuwa itarudi katika safari zake za kawaida kwa sababu Watanzania wanapenda kupanda ndege za kwao.

Waziri huyo alisema hayo jana wakati akitoa shukrani kwa Rais John Magufuli kwa kufungua mkutano wa pamoja wa wadau wa siku mbili wa wajenzi wanaohusisha Bodi za Usajili wa Wabunifu Majengo na Makadiriaji Majenzi (AQRB), Usajili wa Wahandisi (ERB) na Usajili Makandarasi (CRB).

Alisema ndege hiyo imeshaachiliwa, tayari kwa kuanza kufanya safari zake, na kwamba serikali inaendelea na ratiba ya kununua ndege nyingine mbili kama walivyokuwa wamepanga.

“Mheshimiwa Rais, ndege yetu imeachiliwa rasmi, najua mtakuwa mnapokea taarifa kutoka kwenye mitandao ya kijamii, lakini kwa mfumo wa kiserikali hii ndio taarifa rasmi,” alisema Kamwelwe.

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro, aliyekuwapo mahakamani, alisema:

“Tanzania imeridhishwa na uamuzi wa mahakama na Rais Magufuli ameshapewa taarifa ya hukumu ya ndege yetu.”

Aidha, katika hukumu hiyo mahakama imemtaka mlalamikaji Steyne aliyepeleka kibali cha kushikiliwa ndege hiyo alipe gharama za kesi hiyo kwa walalamikiwa.

Mlalamikaji huyo ambaye alipata kibali cha kuishikilia ndege hiyo, alisema hajaridhishwa na hukumu na kwamba amekata rufani.

Taarifa zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya kimataifa imeeleza kuwa rufani hiyo inatarajiwa kusikilizwa.

Wakili wa Steyn, alisema: “Tumearifiwa kuwa ACSA (kampuni inayoendesha viwanja vya ndege Afrika Kusini (ACSA) ipo katika harakati za kuiachia ndege. Kama ndege itaondoka Afrika Kusini, mteja wangu atapoteza bima yake, na jambo hili (rufani) linahitaji kusikilizwa kwa haraka.”

Aidha, iliripotiwa kuwa rufani ilianza kusikilizwa jana  katika Mahakama hiyo.

MCHUANO MAHAKAMANI

Wakati wa usikilizaji wa kesi hiyo mahakamani, jopo la wanasheria wa Tanzania waliopelekwa nchini humo walieleza kuwa amri hiyo ilitolewa kimakosa na kutaka iondolewe.

Wakili wa mlalamikaji, Wakefied, alisisitiza kuwa kuna kesi ya msingi ya kujibu na kuitaka mahakama kuangalia vigezo vya madai hayo na kuvitendea haki.

WAZIRI KABUDI

Naye Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi, alisema jijini Dar es Salaam kuwa wanasheria wa Tanzania wakiongozwa na Dk. Ndumbaro wakishirikiana na timu ya wenzao nchini humo wamewezesha ndege hiyo kuachiwa.

“Dk. Ndumbaro alipelekwa Afrika Kusini tangu Jumamosi iliyopita kwa ajili ya kusimamia shughuli hiyo, uamuzi wa mahakama wa kuiachia ndege yetu umetolewa leo (jana) saa nne asubuhi ambapo ni saa tano kwa mujibu wa saa za Afrika Mashariki,” alisema wakati akitoa tiketi za ndege kwa wanafunzi 100 wanaokwenda masomoni Israel.

Alisema ndege hiyo imeachiwa kwa sababu za serikali ya Tanzania na wanasheria wake walizitoa mahakamani.

“Taarifa zaidi zitatolewa baadaye, mahakama leo imesoma hukumu yake baada ya sisi kuwasilisha hoja zetu Jumanne (juzi) kuomba mahakama itengue uamuzi uliotolewa na Jaji aliyesikiliza kesi hiyo bila ya sisi kuwapo mahakamani.

Hayo ni maamuzi ya mahakama yaliyotolewa, lakini utekelezaji wake tutazidi kufahamishana hapo baadaye,” alisema.

Prof. Kabudi alisema serikali inaendelea kufuatilia baada ya uamuzi huo ni nini kitaendelea.

“Ninawashukuru wanasheria wetu waliotuwakilisha kwenye kesi hii wakiongozwa na Naibu Waziri Dk. Ndumbaro na timu ya mawakili Afrika Kusini,” alisema.

BOSI ATCL

Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi, alisema: “Tutaendelea na safari zetu kwa kuwa kesi iliyokuwa mahakamani haituhusu sisi wala hawakulishtaki shirika.”

 

Imeandikwa na Romana Mallya, Mary Geofrey, Mariam Magili na Rahma Kisilwa (Tudarco)

Habari Kubwa