Mapya safari ya Lissu kurejea nchini Jumamosi

05Sep 2019
Enock Charles
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mapya safari ya Lissu kurejea nchini Jumamosi

ALIYEKUWA Mbunge wa Shingida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameahirisha mpango wa kurejea nchini keshokutwa kutoka Ubelgiji kama alivyoahidi.

Lissu  amesema kuwa ameahirisha safari ya kurejea nchini kutokana na kutopata kibali cha madaktari wake.

Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mwanasheria huyo amesema kuwa hataweza kurejea nchini Jumamosi kama alivyosema awali kwa kuwa ana ratiba ya kumuona daktari wake Oktoba mosi mwaka huu na Oktoba 8, mwaka huu.

“Nilisema mwanzoni kuwa nitarudi tarehe 7 Septemba ya mwaka huu ambayo ni Jumamosi hii ya keshokutwa… lakini mpaka sasa sijapata ruhusa ya daktari wangu, daktari wangu ameniambia ataniona tarehe 1 Oktoba na kwa mara ya mwisho tarehe nane Oktoba,” alisema  Lissu alisema

Kuhusu kuapishwa kwa aliyekuwa mbunge mteule wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, ambaye ndie aliyechukua nafasi yake, Lissu amesema hiyo haimpi shida kwa vile suala hilo bado lipo mahakamani na endapo atashinda kesi mbunge huyo mpya atatenguliwa na yeye kurejeshewa kiti chake.

“Hiyo haina athari yoyote kwa shauri lililopo mahakamani… wabunge huwa wanachaguliwa, wanaapishwa, wanatumikia ubunge halafu mahakama ikipata ushahidi kwa aliyetenguliwa alitenguliwa kinyume cha sheria, anafutiwa ubunge,” alisema.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Jumatatu ilishindwa kutoa zuio la muda la kuapishwa Mtaturu baada ya kuahirisha kutoa uamuzi wa kusikiliza kesi ya msingi hadi Septemba 9, mwaka huu, hivyo juzi mbunge huyo mpya aliapishwa ikuwa siku ya kwanza ya Mkutano wa Bunge wa 14.

Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo mbalimbali awali, Lissu alisema kuwa angerejea nchini Septemba 7, mwaka huu akitokea Ubelgiji alipo kwa ajili ya matibabu tangu mwaka jana.

Mwanasheria huyo ambaye amehudumu kama mbunge kwa takribani mihula miwili, alivuliwa ubunge baada ya taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa maelezo kuwa amekuwa mtoro wa mikutano ya Bunge pamoja na kutokujaza fomu za maadili ya watumishi wa umma.

Septemba 7, juzi Lissu alishambuliwa kwa kupigwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana karibu na nyumbani kwake Area ‘D’ jijini Dodoma majira ya mchana akiwa katika gari lake wakati akitoka kwenye kikao cha bunge.

Baada ya shambulio hilo safari ya matibabu ya mbunge huyo ilianzia katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma na baadae alihamishiwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambapo alikaa kwa siku 121 kabla ya kupelekwa Ubelgiji Januari 6, mwaka jana, ambako anaendelea na matibabu.

Habari Kubwa