JPM awasamehe Makamba, Ngeleja

05Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
JPM awasamehe Makamba, Ngeleja

SAKATA la sauti za vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zilizokuwa zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii, limechukua sura mpya baada ya vigogo wawili kati ya waliokuwa wanasikika kuisema serikali kudaiwa kumwangukia Rais John Magufuli.

Rais John Magufuli akizungumza jambo na Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga, baada ya kufungua Mkutano wa Mashauriano wa Mwaka wa Bodi ya Usajili Wabunifu na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Usajili Makandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), na wadau wa sekta ya ujenzi , jijini Dar es Salaam jana.

Vigogo wanaodaiwa kumwomba msamaha Rais ni aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa pamoja wa wadau wa sekta ya ujenzi unaohusisha Bodi za Usajili waWabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Usajili wa Wahandisi (ERB) na Usajili wa  Makandarasi (CRB), jijini Dar es Salaam.

Alisema vigogo hao na wengine walikuwa wakimtukana na sauti zao zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii lakini wawili kati yao (bila kutaja idadi) walijitokeza kumwomba msamaha na kuamua kuwasamehe.

"Nakumbuka hivi karibuni kuna watu fulani fulani hivi walinitukana weee na nika 'prove'(nikathibitisha) sauti ni zao ‘more than hundred percent’ (zaidi ya asilimia 100). Nikawafikiria nikaona hata nikiwaacha wapelekwe kwenye Kamati ya Maadili (ya Chama Cha Mapinduzi- CCM) adhabu itakuwa kubwa, nikaona ninyamaze.

“Lakini wakajitokeza wawili kati yao wakaniomba msamaha, nami nikajiuliza na mimi kila siku naomba msamaha kwa Mungu na nasali ile sala ya baba yetu utusamehe makosa yetu kama tunavyowasemehe wengine.

Nikaona hawa waliokuja kuniomba msamaha na kweli ya dhamira yao nisipowasamehe ni bataki na maumivu makubwa ndani ya moyo wangu,” alisema Rais Magufuli.

“Niliamua nikawasamehe, waliniomba msamaha wakanigusa, nikaona hawa ni vijana bado wanatafuta maisha na mimi nikaamua kuwasamehe nikasahau kabisa.”

Mbali na Ngeleja na Makamba, sauti zingine zilizosambaa ni za makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana na Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe.

Aliwasihi Watanzania kuwa na desturi ya kusameheana kwa sababu wote ni watoto wa Mungu, hivyo wanatakiwa kusameheana na kuwa huru.

Rais Magufuli alisisitiza kuwa wadau hao wa ujenzi nchini wanatakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano na kusameheana ili kutimiza wajibu wao kikamilifu.

“Mtu akikuudhi na kukutukana kiasi gani ni muhimu kusamehe na kuuishi upendo wa kweli wa kusamehe.  Hata ninyi (wataalamu wa ujenzi) sameheaneni na mimi nimewasamehe," alisema.

Nipashe iliwatafuta Ngeleja na Makamba ili kuzungumzia msamaha huo wa Rais, lakini Makamba aliomba apigiwe baadaye lakini hakujibu na Ngeleja simu yake ya kiganjani iliita bila majibu.