Stars yachungulia hatua ya makundi

05Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stars yachungulia hatua ya makundi
  • ***Mbinu za Ndayiragiji zakubalika, wagoma kuingia chumba cha kubadilishia, Msuva asawazisha usiku huku Samatta akifanya...

TIMU ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), imetanguliza mguu mmoja ndani  kufuzu hatua ya makundi ya kuwania kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022 baada ya jana kulazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao, Burundi.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Mashujaa mjini Bujumbura, Burundi, Taifa Stars ilikataa kuingia katika vyumba vya kubadilishia wakati wa mapumziko baada ya kubaini kuchezewa mchezo mchafu, hivyo kupewa maoni na kocha katika benchi kwa muda wote wa dakika 15.

Wenyeji ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake, Amissi Cedric ambaye aliwahi krosi iliyopigwa na Amissi Mohammed na kuwapita wachezaji watatu wa Taifa Stars, Farid Mussa, Jonas Mkude na Gadiel Michael waliokuwa jirani na golikipa, Juma Kaseja.

Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika tano tu baada ya Simon Msuva kuisawazishia Taifa Stars baada ya kuwahi mpira mrefu uliopigwa na Gadiel na kumzidi mbinu beki wa Burundi na kupiga mpira uliotinga wavuni moja kwa moja huku nahodha wake, Mbwana Samatta, akifanya kazi kubwa ya kumzuia beki wa Burundi asiucheze.

Kwa matokeo hayo, sasa Stars inayofundishwa na Mrundi Etienne Ndayiragije ambaye mbinu zake zilionekana kufaulu, inahitaji ushindi wa aina yoyote ama sare tasa ili iweze kutinga hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali hizo za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Dakika 10 za kwanza za mchezo huo ambao makipa wote wawili, Juma Kaseja wa Taifa Stars na Jonathan Nahimana wote wanaichezea klabu ya KMC FC ya jijini Dar es Salaam, zilimalizika bila kuwapo kwa shambulizi kutokana na washambuliaji kukosa utulivu wanapokaribia kwenye lango la wapinzani wao.

Kipa wa Burundi, Nahimana aliinyima bao Taifa Stars baada ya kupangua shuti la Msuva na baadaye kiungo Hassan Dilunga alichelewa kuunganisha krosi iliyopigwa na Samatta dakika ya 16.

Burundi ilijibu shambulizi hilo, lakini mshambuliaji wake, Bimenyimana Be-Fils Caleb ambaye alikuwa amefanikiwa kumpita beki wa Stars, Haruna Shamte alipiga pembeni na kuikosesha timu yake nafasi ya kufunga.

Dakika ya 50 Stars ilikosa nafasi nyingine ya kupata bao baada ya mpira wa 'frikiki' uliopigwa na Samatta kugonga ukuta wa Burundi huku wenyeji hao pia wakipoteza nafasi ya kufunga kwa straika wake, Abdoul Fiston, kupiga pembeni wakati ameshafanikiwa kumtoka Mkude na kubakia peke yake na kipa Kaseja.

Burundi iliwachezesha; Nahimana Jonathan, Diamant Ramazan, Baganamwa Joel, Nsabiyumva Frederick, Nshimirimana David, Kwizera Pierre/ Amissi Mohammed (dk. 3), Bigirimana Gael, Amissi Cedric, Kanakimana Bienvenu, Bimenyimana Bon-Fils Caleb/ Abdoul Fiston (dk. 41), na Berahino Saido.

Tanzania; Juma Kaseja, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Himid Mao, Salum Aboubakar "Sure Boy"/ Frank Domayo (dk. 65), Mbwana Samatta, Simon Msuva na Hassan Dilunga/ Iddi Suleiman "Nado" (dk. 54).

Habari Kubwa