Tamasha la Jinsia lije na suluhu changamoto zaidi

05Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Tamasha la Jinsia lije na suluhu changamoto zaidi

HARAKATI za kupigania haki za wanawake na watoto na makundi mengine kama watu wanye ulemavu ni endelevu nchini na duaniani kwa ujumla.

Ni makundi yanayohitaji utetezi kutokana kuathiriwa na mambo mbalimbali katika jamii, kubwa kuwanyima haki zao za msingi kama elimu, umiliki wa rasilimali, ikiwamo ardhi na ushiriki katika maamuzi, kwa kutaja baadhi.

Kwa miaka kadhaa wanawake wamekuwa nyuma kutokana na mila na utamaduni katika jamii zetu kuwabagua kwa kuwanyima elimu katika umri wa kusoma, hivyo kuwakosesha fursa ya maendeleo maishani.

Wanawake leo hii wanaendelea kukwama kupata maendeleo kutokana na mila na utamaduni kuwanyima haki ya kumiliki ardhi ambayo ndio msingi wa maendeleo pamoja na kurithi mali.

Kikwazo hiki kinawanyima fursa wanawake wengi kujiendeleza kwa kufanya shughuli za kujiongezea kipato hususan za ujasiriamali, ambazo zinampasa kuwa na dhamana ya kupata mkopo kutoka taasisi za fedha na benki.

Kundi hilo kukosa uwakilishi katika vyombo vya maamuzi kimekuwa kilio kwa kuda mrefu kutokana na uamuzi wa sera, mipango na sheria kutungwa bila kushurutishwa, hivyo kutowatatulia changamoto zinazowahusu.

Vile vile, wanawake, watoto na watu wenye ulemavu wamekuwa waathirika wakuu wa matukio ya ukatili kama kuuawa, kubakwa, kulawitiwa, kutelekezwa, kuteketwa na mengine mengi ambayo kimsingi yanakiuka utu wa binadamu.

Hata hivyo jitihada kadhaa zimekuwa zikifanyika kukabiliana na changamoto zote tulizozitaja dhidi ya makundi haya kupitia utungaji wa sheria, sera na kutekeleza mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo nchi yetu imeiridhia.

Kwa kuwa jitihada hizo ni endelevu, tunatarajia kuwa Tamasha la Jinsia linalotarajiwa kufanyika nchini mwezi huu, litakuwa sehemu sahihi ya kuzipitia, kuzijadili na kufanya tathmini kuhusiana na changamoto hizo kwa lengo la kuhakikisha kuwa zinaendelea kutatuliwa na kuyapunguzia mzigo wa kunyanyaswa, kufanyiwa ukatili na kuyanyima fursa makundi hayo.

Tamasha hilo ambalo huratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) na kufanyika nchini kila baada ya miaka miwili linalotarajia kufanyika kuanzia Septemba 24 hadi 27, mwaka huu,  tunatarajia kuwa limefanyika miaka 25 tangu kuanzishwa kwa mtandao huo, hivyo litakuwa na masuala mengi ya kujadili kwa lengo la kumkomboa mwanamke.

Tunasema hivyo kwa kuwa matamasha haya yamekuwa yakiwakutanisha wanawake kutoka kila pande za dunia wakiwamo waliopata mafanikio makubwa kujadili masuala ya kuwakomboa pamoja na mtoto wa kike, hivyo kuna umuhimu wa kufanya maandalizi mazuri ikiwamo kuandaa vizuri ajenda za kujadili.

Ajenda hizo zijikite zaidi katika hali halisi ya changamoto zinazowakabili wanawake na mtoto wa kike nchini na kuja na maazimio ambayo yatakabidhiwa kwa serikali ili yatekeleze katika kutunga sera, sheria na uaandaaji wa mipango na mikakati ya maendeleo.

Tunatarajia kuona Tamasha hilo likileta matokeo chanya katika ukombozi wa mwanamke kutokana na mabadiliko katika maendeleo ya wanawake yaliyoletwa na Mkutano wa Nne wa Wanawake Duniani uliofanyika Beijing nchini China mapema

miaka ya tisini.

Habari Kubwa