Masanduku huduma ya kwanza kwenye mabasi, malori ni aibu

05Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Masanduku huduma ya kwanza kwenye mabasi, malori ni aibu

HUDUMA ya kwanza huwa ni ya haraka anayopewa mwathirika wa ajali au ugonjwa wa ghafla.

Katika mazingira ndani ya mabasi, imeonekana kuwa ni ya hatari, kutokana na masanduku kubeba dawa zilizopitwa na wakati, pia kuwa na nyembe zenye kutu.

Madhumuni ya huduma hiyo ni kulinda maisha, kusaidia kufufua na kuzuia madhara ya namna hiyo, mpaka huduma ya kamili ya kidaktari itakapopatikana kwa kwenda hospitali au nyumbani kwa majeruhi.

Lakini ushuhuda wa kilichopo kwenye mabasi ni hatari, kwa kuwa hizo dawa au huduma atakayotakiwa kupewa mtu, inakuwa ngumu kuipata, kutokana na hali mbaya ya masanduku na vilivyomo ndani yake.

Masanduku ya huduma ya kwanza kwenye mabasi ya abiria na malori yana dawa zilizopitwa na wakati, nyembe zenye kutu na dawa zimemwagika ovyo.

Pia kuna kashfa wamekutwa nayo baadhi ya waendesha malori, kwamba masanduku yao yamejazwa kondomu.

Katika uhalisia unaotakiwa, sanduku la huduma ya kwanza linapaswa kuwa na ‘plaster’ au bandeji zinazonata, zikiwa salama kwa ajili ya kufunga vidonda na ‘gauze’ safi na salama ya kufunga majeraha makubwa, majisafi na salama, kripu bandeji, mkasi na dawa za kuzuia maumivu.

Sanduku hilo linapaswa kuwa na bandeji za pembe tatu, mipira ya mkononi (gloves) na ‘tweezer’ kwa ajili ya kuondolea vipande vya vitu kwenye ngozi.

Hiyo inaambatana na kuwapo daftari dogo la kuandikia huduma iliyofanyika, tarehe na saa husika, pia spiriti, pamba, sindano au pini.

Nsema katka magari yetu, hali ni tofauti sana.  Katika ukaguzi mdogo uliofanywa kwenye kituo cha mabasi yaendayo mikoani, kilichoko Igambilo mkoani Iringa, ilibainika masanduku hayakuwa na uwezo wa kumsaidia abiria anapopatwa na dharura ya ugonjwa, kwani vyote ndani yake vilikuwa vimepitwa na wakati.

Koplo Faustina Nduguru kutoka Kitengo cha Elimu kwa Umma, Makao Makuu ya Kikosi cha Usalama Barabarani, anasema amekumbana na dawa kuhifadhiwa kwenye mabakuli ya vyakula na zimepitwa na wakati, huku magari hayana kabisa masanduku aina hiyo.

Mwelimishaji huyo, anatumia fursa kusema madereva wanatakiwa kukagua masanduku yao kila wanapoanza safari na kujali uhifadhi wake, ili kuondokana na dhana ya kuweka kitu asikamatwe na wasimamizi wa sheria za usalama barabarani, wakati ndani hakuna vinavyotakiwa.

Koplo Faustina anasema, katika masanduku aliyoyakagua kwa mshtukizo, alikuta baadhi ya dawa zimemwagika na kuwapo chupa tupu.

Anawakumbusha madereva kutambua wajibu wao katika utunzaji masanduku hayo, kwa kuwa ‘kila mtu ni abiria wa kesho’ na atahitaji huduma itokanayo na masanduku hayo, akiwa safarini.

Pia anawakumbusha madereva walichojifunza kuhusu umuhimu na matumizi ya sanduku la huduma ya kwanza na wajibu wa kukikagua kabla ya kuanza safari, lakini wanafanya kinyume, ambao ni uzembe.

Rai yake kwa wamiliki wa mabasi, watambue umuhimu wa masanduku hayo wanayoyatelekeza na mengine yaliwekwa tangu siku gari lilipoanza safari, dawa zake hazijawahi kubadilishwa.

Nitoe rai, hebu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazeee na Watoto, kwa kushirikana na Jeshi la Polisi na wadau wengine, waongeze juhudi ya kutopa  elimu kwa umma, hususan kwa madereva, kuhusu umuhimu wa masanduku yanayotakiwa kuwekwa na aina ya dawa zake.

Najua ndugu zetu wa polisi wa usalama barabarani ambao ndio wadau wakuu walishaanza, nihimize juhudi kuendelezwa zaidi.

Habari Kubwa