Simulizi ya makubwa yaliyojificha kuhusu moto na darasa toka Moro

05Sep 2019
Sabato Kasika
Nipashe
Simulizi ya makubwa yaliyojificha kuhusu moto na darasa toka Moro
  • Kwanini ulipuke, mtaji wake nini?
  • Moto wa gesi ‘janga’ la majumbani
  • Haya ndiyo makundi yake matano

VIUMBE hai vyote vinaufahamu. Binadamu, wanyama na wadudu wanaijua kwa kina na tabia zake.

Kazi ya kudhibiti moto, katika tukio la mjini Morogoro.

Mimea, kupitia tabia ya kimaumbile yake, zaidi inauhisi na kupata athari zake. Lakini, licha ya kuwapo yote hayo, bado inarudi mtihani pale mtu anapohoji tafsiri ya moto ni kitu gani? Ni swali gumu kulidadavua.

Wanasanyansi kitaaluma wamelitolea tafsiri. Kwa  mujibu wa mtandao mojwapo wa unaokusanya kazi za wanasanyansi (sciencelearn.org.nz/resources/7) wanautafsiri moto kuwa  ni matokeo ya hali dhahiri ya kuungua kwa aina fulani ya kemikali.

Hiyo wanaieleza msingi wake unajumuisha hewa ya oksijeni na aina nyingine ya mafuta, ambazo zinapokutana  katika msuguano mkali, zao la mwisho baada ya moto, huwa ni kitu kipya, mathalani majivu.

Watalaam hao wanafafanua zaidi wakisema, ili utokee moto, ni sharti patokee joto kali inayokuwa chanzo cha moto kuwaka. Ni kwa kiasi gani moto huo utadumu?  Inategemea kiwango cha hewa ya oksijeni iliyopo, joto kali na mafuta ndani yake.

Vilevile, anataja kasi ya moto kutokea inategemea nguvu ya msuguano, huku wataalamu wakienda mbali zaidi kwamba, kuna aina ya msuguano huanzisha cheche na kuzaa mlipuko.

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini, ambalo kimsingi ndilo lenye jukumu la kuzima moto na kuokoa maisha na mali katika majanga yatokanayo na moto, mafuriko, tetemeko la ardhi, ajali za barabarani na majanga mengine yanayofanana, nalo lina tafsiri rasmi ya moto.

Inspekta Joseph Mwasabeja, ni Msemaji wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, ambaye katika mazungmzo na Nipashe hivi karibuni, naye kama walivyo wataalamu watafiti, ana ufafanuzi na undani wa dhana ‘moto.’

Anachambua: "Kwanza tufahamu maana ya moto, je moto ni nini? Moto ni muwako unaotokana na mngongano endelevu wa kikemikali na baadaye huzalisha joto na mwanga.

‘Mgongano huu endelevu, ni lazima kuwe na vitu vitatu muhimu ambavyo ni hewa ya oksijeni, joto la kutosha na ‘fuel’ (mafuta), yaani chakula cha moto, ambacho ni kitu chochote kinachoweza kuwaka."

MADARAJA YAKE

Inspekta Mwasabeja anaufafanua moto, kwamba umegawanyika katika madaraja makuu matano, akisisitiza ni muhimu Watanzania kuyafahamu, kwa vile dhana moto ni kitu hatari kwa mali, afya, pia maisha ya watu na viumbe.

Anataja kuwapo Daraja A kuwa ni moto unaotokana na vitu vya asili ya mimea, kama vile karatasi, mbao, nguo na vingine vya aina hiyo.

Pia, anataja Daraja B, kuwa ni moto utokanao na vimiminika vinavyowaka, au ilivyozoeleka na wengi; moto wa mafuta.

"Daraja C, ni moto wa gesi inayowaka na milipuko yote itokanayo na gesi. Moto huo tunauweka katika daraja C na daraja D. Kwenye moto huu, viunguavyo ni vitu vyenye asili ya madini kama vile chuma," anasema.

Msemaji huyo anataja daraja la tano la moto ambalo ni F au K, kuwa unaosababishwa na mafuta ya kupikia yanapochemka sana na endapo yatapata chanzo kidogo cha kisababishi cha moto, huweza kuwaka.

"Hapa ni muhimu nitoe ufafanuzi. Kwanza katika miaka ya ‘80’ kulikuwapo Daraja E la moto ambalo ni umeme, lakini baadaye ikabainika hakuna moto wa umeme, bali umeme ni chanzo kikubwa cha moto," anasema.

Inspekta Mwasabeja anaeleza kwamba, baadaye katika miaka ya 2000, Waingereza waligundua moto Daraja F, ni mafuta ya kupikia na anafanua kuwa nchini Marekani linaitwa daraja K.

KUEPUKA AJALI

Inspekta Mwasabeja, anasema gari lolote lenye shehena ya mafuta linapoanguka, busara ni kwamba halipaswi kukaribiwa na mtu asiye mtaalamu vita dhidi ya moto.

Anafafanua tahadhari haiishi katika mafuta pekee, bali bidhaa nyinginezo zinazosafirishwa katika mfumo wa sumu na kemikali hatari.

Mtaalamu huyo anataja mbinu hiyo ndio sahihi zaidi, inayosaidia usalama wa watu dhidi ya kusogelea eneo lenye ajali, kwa lengo la kuiba au kushuhudia, badala yake wakae mbali kutoa taarifa kwa mamlaka husika.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, mara inapotokea ajali, watu wanatakiwa kuwa umbali wa mita 500 (nusu kilomita ) kutoka eneo la tukio na kupiga simu namba 114, ili mamlaka ziweze kuchukua hatua haraka.

"Zimamoto inapofika kwenye eneo la tukio, huweka alama za onyo kuanzia umbali wa mita 25 kutoka ilipo ajali ili kwamba hata ukitokea mlipuko, basi iwe rahisi watu kusalimika," anasema Inspekta Mwasabeja.

Anafafanua kuwa, hayo yanafanyika ili kutenganisha eneo salama na hatari, lakini anaeleza masikitisho yake watu badala ya kuzingatia maelekezo hayo, baadhi wanakimbilia ajali ama kwa kujineemesha au kushuhudia tukio.

Ushauri wake, ni vyema jamii ikazingatia elimu inayotolewa, kuhakikisha wanakuwa salama na mali zao badala ya kujiingiza kwenye majanga, ambayo mwisho wake si mzuri.

"Vilevile, mbali na kuchota mafuta baada ya lori kuanguka, pia wanatakiwa kujua matumizi sahihi ya majiko ya gesi badala ya kufanya kienyeji, kwani nayo ni hatari iwapo mtumiaji hatazingatia maelekezo," anasema.

MITIHANI GESI

Inspekta Mwasameja anafafanua kuwa, gesi lenye mtungi, ni muhimu mtungi uwe nje huku nyaya zake ndizo zinazoingia ndani ya nyumba.

Ushauri mwingine wa kitaalamu, ni kwamba kwenye majiko nyaya zake zinapaswa kutumika kwa muda si zaidi miaka miwili kisha zinunuliwa mpya.

Majiko yasiyo na mitungi je? Ushauri wake, wapikaji watumie nje, kwani ni hatari gesi kujaa ndani ya nyumba.

Pia, ndio maoni ya Inspekta Mwasabeja, kwa wanaotumia majiko ya mkaa wapikie nje kwa ajili ya usalama wao, akiongeza hata hewa itokayo si salama.

Wataalmu wa elimu ya matumizi ya gesi wanadokeza kuwapo kasoro katika biashara ya gesi zikiwa na upungufu, unaopaswa kufanyiwa kazi na mteja.

Nao wakufunzi kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, wanashauri mtu anaponunua gesi na kuifikisha nyumbani asubiri kwa wastani dakika 30 hadi 45, ili gesi itulie kwanza kutokana na misukosuko ya ubebaji kabla matumizi.

Watumiaji majiko hayo, pia wanapewa mbinu za kubaini wizi unaofanywa na wajanja wachache wauza gesi kwamba ni kuweka mtungi kwenye dyaba lenye maji au jiko dogo la gesi kwenye ndoo ya maji.

"Kama mtungi utakuwa haijajaa gesi, utaelea kwenye maji na kama jiko nalo litakuwa halijajaa, litaendelea, pia kama mtungi utakuwa umetoboka itakuwa ni rahisi kubaini," anasema.

AJALI NCHINI

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, linasema kumekuwapo na ajali za moto katika maeneo mbalimbali na hasa ule wa Daraja B, unaotokana na vimiminika vinavyowaka.

Inspekta Mwasabeja, anatoa mfano mwaka 2002 ilitokea ajali ya moto wa mafuta katika eneo la Ideweli mkoani Mbeya na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30 na wengine 100 walijeruhiwa, baada ya gari kupata ajali na wao kuchota mafuta.

Anataja nyingine ilitokea mwanzoni mwa mwezi uliopita  mjini Morogoro na kusababisha watu zaidi ya 100 kupoteza maisha na kadhaa bado wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini.

Msemaji huyo wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, anasema Watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na historia kwa kuwa tukio la moto si mara ya kwanza.

"Matukio kama hayo yanapotokea hasa ya magari yanayobeba mafuta na kemikali ni hatari, hatutakiwi kuyasogelea isipokuwa wataalamu kwa ajili ya kuondoa hatari iliyo mbele," anasema.

Wakati  vifo vya Morogoro vinaendelea kuombolezwa na majeruhi wanauguzwa, Agosti 25 mwaka huu kuna ajali nyingine ya lori la mafuta ilitokea eneo la Benako, Ngara mkoani Kagera na watu wakakimbilia kwenda kuchota mafuta.

Inaelezwa, kwa bahati Polisi mkoani humo waliwahi kuwadhibiti.

Kwa sasa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Elisha Gaguti, ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani kuwasaka wote waliohusika kuchota mafuta kwenye lori hilo.