Kashfa ngono watoto ilivyomtupia mzigo wa kuhamia jela miaka sita 

05Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kashfa ngono watoto ilivyomtupia mzigo wa kuhamia jela miaka sita 
  • Wapo walioibua madai zama;1961 na 1969 
  • Alipohojiwa alizibeba lawama za waumini
  • Mdau vita ya vijana, Ukimwi, ndoa, mimba
  • Alisakata kabumbu hadi siku ya upadrisho

NI wiki mbili au nusu mwezi uliopita kamili, kwa maana ya siku 15 sasa zimepita tangu msumari wa kisheria kuendelea kupigilia hukumu ya jela miaka sita, kwa Kardinali George Pell wa nchini Australia, akihusishwa na udhalilishaji watoto.

Hiyo ni baada ya kutupwa kwa rufani yake kutokana na hukumu aliyopewa wastani wa nusu mwaka uliopita.

Ni hali inayotafsiriwa kuingia katika rekodi kuwa kiongozi wa juu zaidi wa kanisa hilo duniani kukumbwa na kashfa nzito ya namna hiyo, hadi hatua ya hukumu kisheria, huku ikibeba sura ya pigo kwao.

Akiwa ametumikia nafasi ya Askofu wa Jimbo la Sydney tangu mwaka 1996 na kupandishwa cheo kuwa Kardinali mwaka 2003, Pell, mwenye umri wa miaka 78, shitaka na hukumu yake inaangukia katika kuwajibika wa udhallishaji watoto kingono.

Mnamo Juni mwaka 2017, ndipo alipoanza kusomewa mashitaka mahakamani na baada ya kesi kuendeshwa, Desemba mwaka jana, alitiwa hatiani kwa mashitaka matano yanayohusu udhalilishaji wavulana, matendo yanayoelezwa kutokea katika miaka ya 1990.

Hatimaye, Machi13 mwaka huu, Jaji Peter Kidd wa Mahakama ya Victoria, nchini Australia, alimhukumu kifungo jela miaka sita, ambayo haina fursa ya kisheria kupatiwa kifungo cha nje kupitia msamaha wa parole.

Kardinali hakuridhika, aliwasilisha rufani kupinga hukumu hiyo na ilisikilizwa kwa siku mbili, mwezi Juni mwaka huu na uamuzi wake wa tarehe 21mwezi uliopita, uliridhia hukumu ya awali kwamba aendelee kutumikia kifungo kwa adhabu ileile

Mambo yalivyomgeuka

Tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000, kulianza kuwapo vuguvugu la kashfa kwa kanisa, jamii kupitia vyombo vya habari na mitandao ya jamii ilichachamaa, hata kanisa kuanza kulifanyia kazi. Wakati sakata lilipoanza kuibuka mwaka 2002, aliyekuwa kijana wa miaka 12 mwaka 1961 (wakati analalamika alikuwa na miaka 41), alidai kudhalilishwa katika kambi ya vijana jijini Melbourne. Hata hivyo, aliondoa dai lake, kwamba lishughulikiwe na kanisa.

Baadaye ilishika sura pana, wanaharakati wakija juu na wanasiasa kama kawaida yao nao wakadakia hoja, moto ukawa mkubwa pale ilipokuwa hoja bungeni.

Ni jambo lililotokea, huku Kardinali Pell akizidi kukwea vyeo vya kanisa, hata akafikia kukasimiwa baadhi ya madaraka muhimu katika makao makuu ya Kanisa, ikiwamo kuingoza Sekretarieti ya Uchumi.

Mwishoni mwa 2012, serikali ya Australia iliunda tume kufuatilia kashfa hiyo na Kardinali Pell, akalipokea kwa tamko: “Nadhani ni fursa kuwasaidia wahanga, pia nafasi ya kusafisha hali ya hewa, kutofautisha kashfa na uzushi na kampeni ya vyombo vya habari dhidi ya Kanisa Katoliki.”

Akizumgumza katika hotuba yake ya Krismasi mwaka huo, Kardinali alirudia kuwaomba radhi waathirika na akwaambia Wakristo wawasaidie walioumizwa na jinai hiyo kubwa ya udhalilishaji.

Tume iliendesha vikao vyake kati ya mwaka 2013 na 2017 na Kardinali Pell alitoa ushahidi mara kadhaa.

Mnamo Mei 27, 2013 Kardinali Pell, alitoa ushahidi mbele ya Kamati ya Bunge iliyofuatilia kashfa hiyo ya kuwadhalilisha watoto kutoka katika mhimili wa kanisa na mashirika mengineyo.

Katika majibu na ufafanuzi wake, kiongozi huyo alitamka: “samahani na samahani sana.” Alikiri kashfa hiyo inamuangukia katika nafasi yake ya kulea kanisa.

Ushahidi aliutoa Machi 2014, akiwa jijini Sydney na kupitia mazungumzo ya video kutoka jijini Vatican, Agosti ya mwaka huo; pia kati ya Machi na Februari mwaka 2016.

Mmoja wa walalamikaji anayedai kudhalilishwa mwaka 1969, katika shule moja ya msingi chini ya usimamizi wa pell, alidai kiongozi huyo alimsikia akilalamika kuomba msaada, lakini hakufanya hivyo.

Hata hivyo, dai hilo lilitupwa baada ya Pell kujitetea kwa kutoa ushahidi wa pasi ya kusafiri, unaothibitisha kipindi cha dai la kashfa hakuwapo nchini Australia. Tume ililitupa dai hilo.

Kiongozi huyo aliangukiwa na kashfa nyingine ikimhusu alipokuwa Askofu wa Sydney, iliyohusishwa na udhalilishaji watoto 55, mzizi wa kashfa ukiangukia wakati hajapewa uaskofu.

Mwishoni mwa mwaka 2012, serikali ya Australia iliunda tume kufuatilia kashfa hiyo, ambayo Kardinali Pell kwa upande wake alipokea kwa tamko: “Nadhani ni fursa kuwasaidia wahanga; nafasi ya kusafisha hali ya hewa na kutofautisha kashfa na uzushi na kampeni ya vyombo vya habari dhidi ya Kanisa Katoliki.”

Kardinali Pell, akitoa ushahidi katika vikao vitatu, mnamo March 2014 akiwa jijini Sydney na kupitia mazungumzo ya video akiwa jijini Vatican, Agosit 2014; pia kati ya Machi na Februari, mwaka 2016 nchini  humo mwaka.

Katika ufafanuzi wake wa kikao cha mwaka 2014. Alieleza kwamba Kanisa Katoliki ni sawa na kampuni ya usafirishaji, akitumia mfano: “Kama dereva wa gari akampakia mwanamke na akamdhalilisha, sidhani kama ni sahihi kuuwajibisha uongozi wa kampuni.”      

Ni hoja iliyouamsha Umoja na Wazazi wa Watoto Waathirika wa Udhalilishaji, kupitia Rais wao Cathy Kezelman, aliyekuja juu ‘kuponda’ utetezi huo kwamba unazidi kuwavuruga, huku wenzake wakiunga kupitia mitandao ya jamii, wakitumia  mawazo yanayofanana nayo.

Katika utetezi wake alipokuwa jijini Roma kati ya Februari na Machi 2016 akiwa katika hoteli moja, mbele ya watoto 15 waathirika na kuonyeshwa moja kwa moja kwenye televisheni, Pell aliapa kwa Biblia, akikiri kuwapo kosa.

Hata hivyo, alisisitiza tukio halikuwa na uhusiano wote na makusudi ya kanisa lake, akifafanua:"Kanisa limefanya kosa zito na inafanyia kazi marekebisho.”

Baada ya kuhojiwa katika makao makuu ya kanisa hilo jijini Roma, Juni 2016 kupitia taarifa ya Kurugenzi ya Habari, ilitangaza Kardinal Pell kuendelea na nafasi yake ya Mkuu wa Sekretarieti ya Uchumi ya Kanisa.

Makao makuu ya kanisa, ilikataa kutoa kwa matamshi, ikiahidi kufanya hivyo baada ya kesi kwisha

Afya yake

Huku akiwa katika msukouko wa shitaka dhidi yake kutoka upelelezi wa Polisi, Kadinali Pell ndani ya kipindi hicho alifanyiwa ziara katika makao makuu ya kanisa,Vatican Roma, alikoripotiwa kuugua ghafla.

Shida hiyo ya kiafya aliripotiwa kuipata mnamo Januari 2010, hata akalazimika kwenda makao makuu ya kanisa kuhudumiwa kiafya.

Ni suala lililozua mjadala kisheria, ukiwapo msukumo wa kisheria uliomhitaji nyumbani. Madaktari waliomtibu, walituma ripoti maalum iliyoeleza afya yake na kwamba hakufaa kusafiri angani, wakiahidi angetarajiwa kuwa nafuu ifikapo Februari 2016. Mamlaka za kisheria ziliridhia.

Aliporejea Australia, mashtaka dhidi yake yaliendelea, akifanyiwa ukaguzi maalum kiafya ya mwili na akili akatiwa rumande wakati kesi inaendelea.

Hata hivyo, Desemba mwaka jana alipatiwa dhamana maalum kutoka gereza la Melbourne alipokuwapo, kwenda kwenye tiba ya figo.

Afya na familia

Msimamo wa jamii ya vijana ambao wamemuangushia katika mikono ya sheria, kwanza ana historia nao hadi kufikia hatua kufanikisha kufanyika tamasha lao nchini Australia mwaka 2008, ikiwakusanya watu milioni 500 jijini Sydney.

Kutoka mkusanyiko huo alitoa kauli ya kuomba msamaha kwa niaba ya kuwapo vitendo vya aina ya udhalilishaji kufanyika na aliowaita ‘baadhi ya waumini.’

Huko nyuma katika misimamo yake ya kikanisa, alikemea kitendo cha wanandoa kitengana na athari zake. Mwaka 2001 alipozungumza na radio moja, Pell wakati huo akiwa askofu, alihimza ubaya wake, hasa kwa wanandoa wenye watoto.

Alielekeza maoni kwamba ndoa, ivunjike katika mazingira ya lazima kama vile ukiukwaji wa faragha ya wanandoa na akawa na orodha ya adhabu inayosaidia kulinda uhusiano wa kifamilia.

Kuhusu suala la kuwapo ushoga, mwaka 1990 alitamka kwanza anatambua kuwapo kwake, huku akiweka msimamo wa kutokubaliana nao huku, akiipa heshima mabaya kwamba “ni sumu mbaya kuliko sigara.”

Ni eneo aliloenda nalo mbali, wakati, mwaka 1998 alikataa kuwalisha mkate kanisani ‘mashoga’ kanisani na miaka miwili kabla ya hapo, aliipinga azma ya serikali ya nchi yake kutaka kutunga muswada wa sheria inayowaruhusu mashoga kuasili watoto

Mnamo mwezi Februari mwaka 2007, Kardinali Pell, katika eneo lake la utawala alikemea tabia ya watu kutangaza mabaya ya marehemu wanapokuwa katika taratibu za mazishi na maziko, badala yake alihimiza utaratibu wa kikanisa kwamba ni wakati wa kutoa wasifu bora unaomhusu marehemu.

Ukimwi na ngono

Kadinali Pell mwaka 2009 alijitokeza tena katika namna nyingine kuhusu vita dhidi ya Ukimwi, pale alipoungana na  kiongozi wao mkuu, Papa Benedict wa 16, anayesimamia hoja ya mafunzo kanisa hilo kwamba, kupungua maradhi hayo daima hakutapatikana kupitia kinga ya kondomu.

Anaangukia msisitizo wa ndoa au kuacha vitendo hivyo, akiponda kinga kwamba inamhimiza mtu kutokuwa na tabia ya kuendekeza ngono na kushindwa kuchagua mwenza.

Hata hivyo, katika mtazamo wa namna ya pili ambayo alionekana kuongeza makali ya hoja yake kwamba, wakati wao wana kanisa huanza kwa kugawa kondomu ikiwa hatua ya awali kuibadili tabia.

Katika vita ya kutetea usalama wa mazingira naye amekuwa mstari wa mbele, katika moja ya hotuba zake akiwashambulia Wapagani wa Bara la Ulaya wanachangia uharibifu wa mazingira.

Katika suala la mapenzi ya jinsia moja amekuwa mkali, akikemea, tangu mara alipoingia katika nafasi yake alikumbukwa mwamzoni mwa mwaka 2000, kwamba ni ukiukwaji wa amri 10 za Mungu.

"Mafunzo ya Kikristo kuhusu mapenzi ya  ngono, ni sehemu ya amri 10 za Mungu na muhimu kwa ajili ya afya ya mwanadamu,” anasema Kardinali Pell, akitaja maeneo muhimu kama ndoa na familia.

Historia yake

Kardinali Pell, alizaliwa Juni 8, mwaka 1941 nchini Uingereza, akiwa mtoto wa muumini wa dini ya Kianglikana na mama yake ndiye alikuwa Mkatoliki.

Maisha yake ya ujana, katika ya mwaka 1956 na 1959, baada ya shule alikuwa msakata kabumbu maarufu, hata kuwahi kusajiliwa na vilabu vya Richmond na baadaye VFL, nchini Australia.

Kwanini aligeukia upande wa dini? Ana ufafanuzi: “…Nilihofu, nikashuku na hatimaye nikashawishika Mungu ananihitaji kufanya kazi yake."

Huku akiwa hajaupa kisogo kikamilfu, mwaka 1960, alianza mafunzo rasmi ya dira na mwaka 1963 alipatiwa nafasi zaidi ya kwenda kusoma ngazi ya shahada huko Roma, Italia ambako ni makao makuu ya kanisa hilo.

Huko hakuweka kando usakataji soka, hadi pale alipohitimu masomo na kupatiwa upadrisho, mnamo Agosti mwaka 1966.

Baada ya hapo alitumikia kanisani kwa mwaka mmoja, 1967, aliporudi darasani katika Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza na mwaka 1971, alitunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Historia ya Kanisa.

Kardinali Pell ni mpenda vitabu na darasa, kwani baada ya kuwa kazini, hadi kufikia mwaka 1982 alisharudi na kutunukiwa shahada ya juu ya elimu, katika Chuo Kikuu, cha Melbourne

Nchini Australia, ni kipindi hicho alitumikia uongozi wa vitengo vya elimu kanisani, kati ya mwaka 1973 to 1983, ikiwamo kuongoza chuo cha kanisa kati ya mwaka 1973 na 1984, pia wakati huo huo mhariri wa jarida, kati ya mwaka 1979 na 1984.

Mwaka 1987, ndipo alipoteuliwa kuwa msaidizi wa askofu na miaka tisa baadaye, aliteuliwa kuwa Askofu wa Melbourne nchini Australia mnamo mwaka 1996, baadaye mwaka 1997 alihamishiwa jijini Sydney, Juni 2001.

Kwa mujibu wa taarifa za kimataifa zinazomhusu mlalamikiwa.