Sekta viwanda, fedha zaanza kutafutana

06Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Sekta viwanda, fedha zaanza kutafutana
  • Paundi yaporomoka; hofu zatawala
  • Johnson ahaha, kizingiti ‘backstop’

VIWANDA nchini Uingereza vinalalamika kushuka uzalishaji tangu mwaka 2012, tangu kipindi cha kumalizika msukosuko wa sekta ya fedha duniani wa 2008. 

• James Gordon Brown, mkereketwa wa mada ya Brexit na Waziri Mkuu Mstaafu.

Mtazamo ni ‘oda’ ya bidhaa, kwa maana ya mahitaji ya kutengenezewa bidhaa na kupelekewa kwa wateja, zimeshuka kwa kiwango kikubwa ndani ya miaka saba iliyopita, wataalamu wakitafsiri kupitia msemo:“sekta ya biashara inajisikia vibaya, hadi suala la Brexit litatuliwe.”

Sarafu ya Uingereza ambayo kwa kawaida ni zaidi ya Dola ya Marekani kwa kiwango mara moja na nusu, ilishuka kufika wastani wa 1.2 dhidi ya dola, hivi karibuni.

Watalaamu walikuwa wanajiuliza kama hali hiyo ya kukosa imani na shauku ya kuzalisha katika viwanda itadumu au itaanza kupotea baada ya Brexit kulamilika Oktoba 31.

Kuna suala moja katika mchakato mzima wa Brexit linaloendelea kujadiliwa, kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya (EU), ni kinachoitwa ‘backstop’ ambao ni mpaka wa Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland kubaki wazi, kwa kiasi kikubwa.

Hilo ni eneo linaloleta wasiwasi mkubwa kwa serikali ya Uingereza na  Ulaya, hivyo Ujerumani na Ufaransa zinatafuta njia ya kulitatua.

Kwa mengine yaliyobaki, hakuna kitakachojadiliwa kati ya serikali ya Waziri Mkuu Boris Johnson na EU. Hivyo, uwezekano wa kutoka bila mkataba upo, labda mkataba uliopo uboreshwe kuhusiana na hiyo ‘backstop.’

Ukifikiwa muafaka kuhusu mpaka, sehemu ya mzozo wa  Brexit utapungua na Waziri Mkuu Johnson, anaweza kupitisha muswada wa sheria kujitoa EU, kama kanuni rasmi, ili mradi aungwe mkono na kundi la Ireland ya Kaskazini.

Hata chama cha kizalendo cha Scotland, nacho kinaweza kuafiki, licha ya kwamba zaidi ya upande wa chama cha Labour, kupinga ‘Brexit.’

Inaangaliwa kwamba, maelewano yakipatikana,  yatapunguza ugumu wa serikali ya Johnson kuweka mikakati ya kibajeti (ikiwamo bajeti ndogo ya dharura kuelekea mwisho wa mwaka) kutatua mikwamo inayoweza kutokea, Brexit itakapokamilika.

Hata hivyo, bado hakuna uhakika ni wa kiasi  cha mkwamo Uingereza au kusitasita uzalishaji viwandani na kuzorota thamani ya fedha, kunakotokana na Brexit, vivyo hivyo, kwa nchi za Ulaya.

Kunatathminiwa kwamba ‘kiwingu’ cha kupungua ukuaji  uchumi kutokana na vita ya kibiashara, kati ya Marekani na China na hata au upungufu wa mauzo nje, kutokana na vikwazo Marekani inavyolazimisha kwa Iran.

Pia, EU imejiwekea vikwazo vya kibiashara dhidi ya Russia, ambayo ilitengwa kutoka kudi la mataifa tajiri duniani maarufu G8, kutokana na uvamizi wa Crimea, eneo la Kaskazini ya Ukraine lenye raia wengi wanaozungumza Kirusi.

Dira soko

Watafiti wa uchumi, wanasema soko la dunia hivi sasa linajikongoja, huku mahitaji ya bidhaa za viwandani kutoka Ulaya kwenda Marekani na bara la Asia yamepungua.

Uingereza inatajwa kuwa na soko kubwa zaidi la bidhaa za viwanda barani Ulaya, lakini kuna watafiti wanaosema, kujitoa bila mkataba, kutasababisha kero na mkwamo wa bidhaa hizo, kutokana na janga la kodi.

Kuna mchambuzi aliyetumia mfano wa ubashiri, kwamba magari ya mizigo yatapanga foleni kwa siku tatu katika kituo cha Dover Mashariki ya Uingereza, ambako magari hujiandaa kupita katika barabara ya chini ya bahari kuingia Ufaransa. Kwa jumla ni hofu kila kona Ulaya.

Wanunuzi wa jumla wa bidhaa za viwanda, wanaelekeza ‘oda’ zao kwingineko na siyo Uingereza, wakihofia kupanda kodi Uingereza ikigeuka kuwa ‘nchi ya tatu,’ isiyo na uhusiano wa moja kwa moja na unafuu wa kodi.

Takwimu za mwezi Agosti zilionyesha uzalishaji viwandani umepungua, pamoja na mauzo ya nje na kupatikana nafasi za kazi.

Wataalamu wameanza kujiuliza kama uchumi unashuka kwa jumla (recession), kama ilivyoanza kuhofiwa nchini Marekani, kutokana na vita ya kibiashara na China.

Kwa upande wa Marekani, wasiwasi uliondoka muda, lakini Uingereza itapata tabu kujinasua.

Johnson shakani

Mchambuzi mwandamizi, James Gordon Brown, anaitazama kwa tabu serikali ya Johnson, kutokana na vitisho anavyotoa kuhusu kitakachotokea nchini humo Brexit, bila ya kuwapo mkataba ikitekelezwa.

Ni hofu inayotokana na ukweli, Brown ameshika nyadhifa za juu nchini humo, kwani alikuwa Waziri wa Fedha kati ya mwaka 1997 hadi 2007, halafu waziri mkuu kwa miaka minne.

Kwa vile sakata la uchumi duniani lilianza na mkwamo wa mabenki kadhaa katika soko la fedha nchini Marekani mwaka 2007, ulimkuta ndiyo kwanza anaingia katika uwaziri mkuu na akaondoka mkwamo ukiendelea. Hiyo, inadhaniwa kutawala mawazo yake.

Brown ameibua hofu ya kwamba kutakuwapo uhaba mkubwa wa chakula nchini humo, endapo Brexit bila ya mkataba itafikiwa, akitoa mwito wa kuzuiwa kwa Brexit kabla ya majanga kuifika Uingereza.

Akiongea na wafanyakazi katika  kiwanda cha mikate jijini Liverpool, ambako ni kikundi cha ushirika, anasisitiza kuwa umaskini utaongezeka nchini humo, endapo Brexit itatekelezwa kwa hali yake ya sasa.

Brown ni mmoja wanaounga mkono hoja kuwa “mradi Bunge la Uingereza limeshindwa kufikia mkataba wa kujitoa Umoja wa Ulaya, basi isijitoe sasa na ingoje hadi mkataba kama huo ufikiwe.” Ni mchakato ambao chama tawala hakiukubali, pia EU.

Uhaba chakula

Michael Gove, Waziri wa Johnson anayesimamia matayarisho ya kujitoa bila ya mkataba, anasema baadhi ya bei za vyakula zinaweza kupanda, lakini hapatakuwapo uhaba wa aina ‘hiyo au ile’ ya bidhaa za vyakula, kama nafaka, maziwa na nyama. Ni mahitaji ambayo sehemu yake inaagizwa kutoka bara Ulaya.

Hata hivyo, alipotakiwa kueleza hitaji la ongezeko la bei, alifafanua kuwa baadhi ya vyakula vitapanda bei na vingine vitashuka bei, kutokana na kupungua kwa kiasi fulani mwingiliano wa soko la Uingereza na Ulaya kwa jumla.

Brown anatahadharisha kuwa umaskini utazidi, kwani wanaosaidia kutoa vyakula nao watakumbwa na uhaba.

Wachuuzi wa vyakula, ambao wanaagiza zaidi kutoka nchi za EU, wanakana kwa kusema hakutakuwapo uhaba wa vyakula EU.

Lakini, msemaji wa kundi lingine la waingizaji wa vyakula ambalo lina mwelekeo wa chama tawala, anasema kuwa haiwezekani kuondoa athari za kuvurugika kiasi fulani kwa mkondo wa uagizaji bidhaa, kwa sababu vyakula kama nyama na mboga, haziwezi kununuliwa kwa wingi na kuhifadhiwa.

 Ofisa wa kikundi cha kutengeneza mikate alichotembelea Brown, anasema ameshaona malighafi wanazoagiza kwa ajili ya uzalishaji zimeshapanda bei.

Brown anasema, kujitoa EU bila ya mkataba kutaathiri kwa kiwango kikubwa biashara ya magari au viwanda vya kutengeneza magari nchini humo.

Haya hivyo, wapo  wengi wana wasiwasi na anachosema Brown, akidaiwa anaongeza shauku kila kukicha. Mwezi Septemba mwaka jana, alisema ‘dunia haina uongozi’ akimaanisha kuparaganyika kwa dira ya Marekani katika uchumi wa dunia na utandawazi.

Mtazamo wake ni dunia inajongea, taratibu katika mkasa mkubwa wa uchumi kama ule wa 2008. Alirudia tahadhari ambazo hazikuchukuliwa wakati ule, ambazo baadhi ya wanaompinga wanabeza.

Habari Kubwa