Hivi ndivyo Mradi Uendelezaji Dodoma unavyoliunda upya jiji

06Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Hivi ndivyo Mradi Uendelezaji Dodoma unavyoliunda upya jiji
  • Kituoni: Nafasi VIP, mabasi 250,  abiria 3,000
  • Egesho malori 500; taa kona zote; soko kubwa
  • Mapumziko Chinagali ‘yamkosha’ Majaliwa 

TANGU serikali ianze kuhamishia shughuli zake jijini Dodoma miaka minne iliyopita, kumekuwapo utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa.

Ujenzi wa soko la kisasa.

Ni utekezaji na mpango ulioridhiwa mwaka 1975, makao makuu ya nchi na kinachofanyika sasa ni kuwezesha jiji hilo liendane na hadhi yake.

Majiji mengine nchini ni Mbeya, Arusha, Tanga, Mwanza, Dar es Salaam,  sasa Dodoma inatekeleza Mradi wa Uendelezaji Miji Mkakati(TSCP), ambayo imepewa kipaumbele katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali, kutokana na hadhi hiyo.

Miradi wa ujenzi wa kituo kikubwa cha kisasa cha Mabasi yaendayo mkoani, chenye hadhi sawa na uwanja wa ndege.

Ujenzi wa soko kuu la Dodoma kwenye eneo la Nzuguni, pamoja na eneo la mapumziko maarufu kama Chinangali Park, ambayo ujenzi wa miradi hiyo unafanywa kwa mkataba wa ujenzi wa Sh. bilioni 35.4.

Mratibu TSCP

Ujenzi wa miundombinu hiyo, mratibu wa miradi hiyo, Mhandisi Emmanuel Manyanga, anasema jiji hilo limepewa kipaumbele kwenye miradi hiyo, pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ili kulifanya liwe la kuvutia.

Anasema, kituo cha mabasi kina uwezo wa kuegesha mabasi 250 kwa wakati mmoja, huduma mbalimbali za ndani na eneo la kupumzikia abiria zaidi ya 3,000.

Pia, anasema eneo hilo ni la ghorofa hivyo yamewekwa maeneo ya biashara kama maduka, huduma za vyakula, eneo la wafanyabiashara ndogo, vyumba kwa ajili ya kukatia tiketi.

“Pia tumeweka ‘VIP lounge’ (abiria wenye hadhi maalum) kwa ajili ya huduma mbalimbali, pia tutaongeza majengo kwa ajili ya kupata huduma ya malazi kwa abiria wa mikoani,”anasema.

Manyaga anasema, kituo hicho kitakuwa na eneo la malazi kwa ajili ya abiria kwa gharama nafuu na itaendeshwa huduma hiyo na halmashauri ya jiji hilo.

“Hii ni stendi kubwa na nzuri hadhi yake ya kimataifa maana ni stendi kubwa kwa Afrika Mashariki, itatoa huduma za kimataifa,” anasema.

Mtaalamu huyo anasema, usanifu wa kituo hicho wameuchukua kutoka nchi mbalimbali, ikiwamo Dubai na Afrika Kusini.

“Tumeangalia stendi za mikoa mingine tukaona upungufu tukajiongeza hadi kuwawekea vizimba wafanyabiashara,” anasema.

Anaongeza kuwa “Usanifu wa jengo letu umekaa kwa muundo wa ndege mtu akiingia Dodoma akiangalia anaona kama ndege inataka kupaa kumbe ni jengo la stendi yetu.”

Akizungumzia eneo la kupumzikia la Chinangali Park, mtaalam huyo anasema katika eneo hilo kutakuwa na viwanja vya michezo mbalimbali ya wakubwa na watoto.

Kuhusu soko, anasema litakuwa jengo la ghorofa moja na wafanyabiashara zaidi ya 500 wanaweza kufanya biashara zao humo.

Mkurugenzi Jiji

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma, Godwin Kunambi, anasema wanatekeleza miradi hiyo, kwa ufadhili wa serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia.

 

Anasema mradi TSCP unahusisha ujenzi wa miundombinu ya barabara katika maeneo ya Kikuyu, Chidachi, Kinyambwa, Itega, Njedengwa, Mapinduzi, Ilazo, Ipagala, Chamwino, Kilimani, Majengo, Mlezi pamoja na maingilio na Kituo cha mabasi na soko kuu.

 

Mkurugenzi huyo anasema, barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami, pia zitawekwa taa barabarani takriban 925 zinazotumia mfumo wa umeme wa jua.

 

Pia mradi huo unahusisha kituo cha maegesho ya malori makubwa utakuwa na uwezo wa kuwezesha takribani 300 katika eneo la Nala.

 

Anaongeza kuwa mbali na kituo kikuu cha mabasi na soko kuu, pia kuna ujenzi wa vituo sita vya watembea kwa miguu; vizimba saba vya kukusanya taka ngumu; uboreshaji mandhari ya eneo la kupumzika katika eneo la Chinangali.

 

Jingine analolitaja Kunambo ni ujenzi wa mtaro wa maji ya mvua wenye urefu wa kilomita 6.5 katika eneo la Ipagala .

 

Kwa mujibu wa Kunambi, Jiji la Dodoma limepata miradi ambayo inagharimu takribani Sh. bilioni na anafafanua: “Kupitia miradi hii Jiji la Dodoma linaenda kutekeleza azma yake ya maandalizi ya kujitegemea kupitia mapato yake ya ndani, Sh.Bilioni 20 zitapatikana kutoka kituo cha mabasi, soko, maegesho ya malori.”

Kunambi anasema kwa sasa wanategemea mapato kwenye uuzaji viwanja, lakini miradi hiyo ndio mbadala wa mapato ya ndani.

“Kupitia miradi hii tunashukuru serikali kwa kutupatia fedha kwa ajili ya miradi hii, na itasaidia jiji kuwekeza kwenye vyanzo vingine,”anasema Kunambi.

 

Mweka Hazina

Mweka Hazina wa Jiji la Dodoma, Alfred Mlowe, anasema mradi wa TSCP katika mfumo wa ukusanyaji mapato, zimenunuliwa mashine za kusaidia kukusanya 211, ambazo zimeziba mianya ya upotevu wa mapato.

“Kwa miaka mitatu 2016/17 zilikusanywa Sh. bilioni 4.7, mwaka 2017/18  na jiji lilikusanya  Sh. bilioni 24.7 na mwaka 2018/19, limekusanya Sh. bilioni 71 sawa na asilimia 105. Hivyo, utaona mchango wa TSCP ni mkubwa sana.”

Mlowe anasema, vitega uchumi vilivyojengwa kupitia mradi wa TSCP vinatarajiwa kupaisha mapato zaidi kwa mwaka wa fedha 2019/20, kwamba zitapatikana Sh. bilioni tisa, kwa kipindi cha miezi sita na baada ya mwaka mmoja vitaloingizia jiji la Dodoma, zaidi ya Sh. blioni 20.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Profesa Davis Mwamfupe, anatoa wito kwa wananchi kutumia fursa zilizopo kwenye miradi na kuilinda.

“Baada ya Dodoma kutangazwa kuwa makao makuu, mahitaji ni makubwa na kwa bajeti ya jiji, tusingeweza kutekeleza miradi kwa kiasi hiki. Kwa kuwa serikali imechukua jukumu hili, naishukuru sana serikali,” anasema.

Waziri Mkuu

 

Mwishoni mwa mwaka jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitembelea Mradi wa Uendelezaji wa Miji ya Kimkakati katika jiji la Dodoma na alikagua ujenzi wa maegesho ya malori makubwa katika eneo la Nala na uboreshwaji mandhari ya eneo la kupumzikia la Chinangali.

 

Katika hilo, alimuagiza Mkurugenzi wa Jiji, Kunambi, aendelee kutenga maeneo ya mapumziko, ili wananchi wapate sehemu za kukutana, baada ya kumaliza kufanya kazi.

 

Waziri Mkuu anaupongeza uongozi wa jiji Dodoma kwa kubuni wazo hilo na anahimiza umuhimu kwa miji mikubwa kutenga maeneo kwa ajili ya mapumziko na yatumike kwa madhumuni yaloyopangwa .

 

 

“Hatuwezi kuwa tumejaza nyumba kila eneo, watu hawana mahali pa kupumzika na kukutana na marafiki zao. ‘Plan’ (mpango) ya Chinangali Park ni nzuri. Jiji la Dar es Salaam ‘plan ya awali kulikuwa na maeneo ya mapumziko, lakini watu wa Idara ya Ardhi waliyauza,” anasema Majaliwa.

Habari Kubwa