Ndege walivyoteketeza ekari za mtama, alizeti na ufuta  shamba

06Sep 2019
James Lanka
Nipashe
Ndege walivyoteketeza ekari za mtama, alizeti na ufuta  shamba
  • Pata dodoso la mtama unavyokomboa njaa 

HIVI karibuni taarifa ya hali ya uzalishaji na upatikanaji mazao ya chakula nchini, inaonyesha hali imeendelea kuwa nzuri katika miaka kadhaa, kujitosheleza kwa mahitaji.

Mkulima Salum Rashid, akionyesha shamba lake la mtama, lililoharibiwa vibaya na ndege wilayani Mwanga.

HIVI karibuni taarifa ya hali ya uzalishaji na upatikanaji mazao ya chakula nchini, inaonyesha hali imeendelea kuwa nzuri katika miaka kadhaa, kujitosheleza kwa mahitaji.

Kimsingi, tathmini ya hali ya chakula, uzalishaji wa mazao ya chakula na usalama wake, unaangaliwa katika baadhi ya mazao muhimu yanayohitajika zaidi, kama vile mahindi, mtama, ulezi, mchele, jamii ya kunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi.

Katika kipindi hicho, nchini kumekuwapo na kiwango toshelevu kinachovuka mahitaji. Ni mafanikio yanayotajwa kutokana na sababu mbalimbali.

Hiyo inajumuisha, hali nzuri ya hewa, usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali ya kiserikali na wadau wengine wa masuala ya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji.

Wizara ya Kilimo mwezi Mei hadi Juni maka huu, ilifanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2018/2019 na upatikanaji wa chakula kwa kipindi kilichopo cha mwaka 2019/2020 katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kwa lengo la kubaini kiwango cha uzalishaji na mahitaji.

Zao Mtama

Inajulikana, chakula kikuu kwa jamii nchini ni ugali, hasa utokanao na zao la mahindi, inayozalishwa kwa wingi katika maeneo mengi nchini.

Kwa mantiki hiyo, iwapo kutakuwapo upungufu wa zao hilo halitazalishwa kwa wingi, basi taifa linaweza kuingia katika baa la njaa. Mtama unaingia katika suluhisho la tatizo hilo, kutokana na kuhimili ukame.

Mtama inaangukia katika kundi la mbegu, punje ndogo katika jamii ya nafaka, ambayo ina kiasi kikubwa cha kabohaidreti.

Zao hilo kimazingira hilo lina uwezo mkubwa kuvumilia hali ya ukame kuliko mengine ya jamii yake, hali inayoifanya kulimwa katika maeneo mengi duniani, hata penye uhaba wa mvua.

Unga wa mtama hutumika kuandaa ugali, kuoka mikate, kupika ubwabwa na unaweza kuchemshwa na kuliwa.

Viwanda vya bia, navyo hutumia mtama kuwa malighafi kuu, majani na mabua yake yanaweza kutumika inaliwa na mifugo. Pia, mabua makavu yanatumika kujengea mabanda ya mifugo na makazi.

Zipo aina za mtama na mbegu zake. Hizo hutofautiana, kulingana na rangi zake; nyekundu, kahawia, nyeupe zinazojumuisha aina zaidi ya 20 duniani.

Mtama una aina zake. Zipo chachu, hasa mbegu za kahawia na nyekundu, mtamu; hasa rangi nyeupe na wakulima wengi hupendelea kuilima.

Mbegu za kisasa za mtama ni laini kuliko mbegu za asili ambazo unakuwa ‘mtama mgumu’ au ‘mtama wa asili.’

Hizo zina mbegu ndefu kwenda juu na huchukua muda mrefu kupanda hadi kuvuna, kuliko mtama wa kisasa, ambao ni mfupi na huchukua muda mfupi, huku ikitoa mavuno bora zaidi, kuliko ya asili.

Kwa kawaida, mtama ukilimwa vizuri, unatoa wastani wa tani moja hadi mbili na nusu kwa shamba la ekari moja .

Pamoja na uhaba wa mvua za mwaka huu, lakini mtama umo katika mavuno bora.

Ndege wa mtama

Hivi karibuni makundi ya ndege aina ya Kweleakwelea yalivamia mashamba ya mtama, ufuta na alizeti wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro na kuteketeza ekari zaidi ya 40 za mazao hayo na kusababisha hasara kubwa.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wakazi eneo la Kitopeni katika Kata ya Kifaru wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Wanasema makundi hayo ya ndege yalianza kuvamia mashamba mwishoni mwa mwezi Juni iliyopita na mavuno yakiwa yamemea vizuri.

Mkulima wa mtama, Kuria Msuya, anasema ndege hao wamewaletea uharibifu mkubwa, pia hofu ya kuwapo balaa la njaa, badaa ya wakulima hao kukosa mavuno waliyoyategemea.

“Ndege hawa wameharibu mazao yote. Mimi mwenyewe nimelima ekari sita za mtama, nao umeliwa wote. Sikuvuna hata punje moja. Nitoe rai kwa serikali kuingilia kati,” anafafanua Msuya.

Anasema, serikali imekuwa ikihamasisha walime mtama kwa vile linakabiliana na ukame na binafsi kama walivyo wenzake wamelima.

Msuya anasema, amelima ekari sita za zao hilo, lakini ndege aina ya kweleakwelea walivamia shamba lake na kula mtama wote, jambo analosema limenyima mavuno.

Anasimulia:“Kutokana na makundi ya hawa ndege, sijaweza hata kupata punje moja ya mtama kwa msimu huu nililima ekari sita za mtama.

“Ni kuanzia kulima shamba, kuotesha, palizi, ilitumia zaidi ya Sh. milioni tatu katika kuitikia wito huo wa serikali, lakini zote zimeishia chini kufuatia uharibifu uliofanywa na ndege hao.”

Msuya, ambaye ni Diwani wa Kata ya Kileo, anafafanua kwamba ni jambo linalowahatarisha kukata tamaa na vyema serikali kuwasaidia kukabili athari hiyo.

Mkulima mwingine wa eneo hilo, Mohammed Rashid, aliyelima ekari 20 za ufuta, lakini hakuweza kuvuna chochote kutokana na mazao yake kuliwa na wavamizi kweleakwelea.

“Ndege hawa wana akili sana. Licha ya kuweka vijana kwa ajili ya kulinda, bado ndege hawa walivamia mashamba na kula mazao haya,” anasema.

Anafafanua kuwa, ndege hao hutokea upande wa safu ya milima ya Usambara na kuvamia mashamba yao, pamoja na kuweka vijana kulinda mashamba hayo, bado ndege wanavamia na kumaliza mazao yao yote.

Selemani Mfinanga, mkulima wa ekari 10 za alizeti, analalamika kwamba hali ni tete kwa wakulima wa mazao hayo, ambao kweleakwelea wameshambulia mazao yao.

DC Mwanga

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, anakiri changamoto hiyo na kuongeza kwamba, mbali na suala hilo, zipo kero kadhaa za wakulima na wafugaji.

Apson anaahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo na ufugaji katika wilaya hiyo, ili kuziondoa haraka iwezekanavyo.

Habari Kubwa