JPM   alipotoa ‘dozi’ nzito mara alipokabidhiwa SADC

06Sep 2019
Beatrice Moses
DAR ES SALAAM
Nipashe
JPM   alipotoa ‘dozi’ nzito mara alipokabidhiwa SADC
  • Aanika uchochoro wanakokwama
  • Sekretarieti SADC ijitathmini upya  

MWAKA 2015 wakati wa kampeni akiwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, akiwa miongoni mwa wagombea, moja ya vionjo alivyotumia  kunogesha kampeni ilikuwa ni kupiga ‘push up’ na ngoma.

Rais Dk. John Magufuli akisalimiana na Dk.Stergomena Laurance Tax.

Kwa wana  mazoezi wanatambua maana ya ‘push up.’ Ina mchango mkubwa katika kujiweka sawa kiafya na misuli ya mwili, usiwe mlegevu.

Alipotangazwa mshindi na kuapishwa, akaja na kaulimbiu isemayo ‘hapa kazi tu’ ambayo pia ni usemi unaopatikana sana katika nyimbo za mazoezini (…kuruta nyama, aah! hapa kazi tu!...), hivyo hivyo ‘push  up.’

Kauli hiyo ya Dk. Magufuli maarufu kama JPM, ilinogeshwa na ‘push up’ alizotumia, ikibeba tafsiri kwamba mchapa kazi, ni lazima awe shupavu kimwili na kiakili na akiwa mlegevu anaharibu kazi.

Rais Dk. Magufuli hakusita kuwaondoa kwenye nafasi za uongozi viongozi kadhaa, aliowahisi au kubaini kuwa wanafanya kazi kwa ulegevu tofauti na mwongozo wake na msimamo wake tangu kampeni za urais.

Alipokabidiwa SADC

Ilikuwa tarehe 17 ya mwezi uliopita, ndio Rais Dk. Magufuli alikabidhiwa uenyekiti wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoka kwa Rais wa Namibia, Dk. Hage Geingob, aliyetumikia wadhifa huo kwa mwaka mmoja, kama ilivyo kanuni ya chombo hicho.

Wakati anapokaribishwa kuzungumza mbele ya wakuu wa nchi na viongozi wa serikali kutoka nchi 16 za jumuiya hiyo, Rais Dk. Magufuli, kamwe hakuficha hisia zake za maumivu juu ya namna nchi wanachama wa SADC zilivyoshindwa kufikia malengo ya ukuaji uchumi.

Wakati malengo yalikuwa asilimia saba, ambayo  na Tanzania ilifanikiwa kufikia, baadhi ziliambulia asilimia tatu pekee.

Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. Magufuli alieleza haja ya kuimarisha Sera za Uchumi na Fedha kwa nchi wanachama, ili kufanikisha malengo iliyojiwekea.

Akitumia rungu la uanachama na uenyekiti wake, aliiagiza Sekretarieti ya SADC kujitathmini, kwani bado haijaonyesha mchango wake kuwa na mwongozo mzuri unaozisaidia nchi wanachama, kufikia hatua za mafanikio kiuchumi.

“Hakuna sababu ya kuficha bado sekretarieti ya SADC haijanifurahisha, takwimu za kiuchumi zimekuwa zikishuka siku hadi siku na sekretarieti haina msaada unaotosha. Hii ni changamoto kwenu ninyi na mjitathimini,” Rais Dk.Magufuli alitamka katika mkutano huo.

Ni kauli iliyopokewa kwa shangwe na wajumbe wengi waliohudhuria mkutano huo, unaofanyika mara moja kila mwaka katika nchi inayopangwa kuwa mwenyeji.

Sekretarieti hiyo, inaongozwa na Katibu Mkuu wa SADC, Dk.Stergomena Laurance Tax, Mtanzania, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara, ambaye katika hatua nyingine ya hotuba, alimtangaza mwanamke wa Kitanazania mahiri.

Awali, alipofungua Maonyesho ya Viwanda Kwa Nchi za SADC, ikiwa ni hatua ya utangulizi ya mkutano wa wakuu wa nchi, Rais Dk. Magufuli, alibainisha viwanda ni eneo muhimu la uwekezaji katika ukuzaji uchumi, kwa kuwa ndiyo inayoongeza ajira na kutokomeza umasikini.

Dk. Magufuli anasema, historia kutoka mataifa yaliyoendelea, unaonyesha ni lazima kupitia mapinduzi ya viwanda, ili kufanikiwa katika uchumi, badala ya kuwa mwagizaji bidhaa, nchi inapokuwa mzalishaji na muuzaji, inaweka ushindani wa kibiashara sokoni.

“Mchango wa sekta ya viwanda katika nchi za Afrika na SADC bado ni mdogo sana. Sekta hii inachangia wastani wa asilimia 10 ya pato la taifa na katika jumuiya ya SADC, inachangia asilimia 11 pekee,” anasema.

Rai ya Dk. Magufuli ni kwa SADC ijikite katika kukuza na kuendeleza ubunifu, ikiwamo kuendeleza teknolojia rahisi ya viwanda, kuwaendeleza vijana na viwanda vidogo.

“Ukosefu wa viwanda unaifanya Afrika iendelee kuwa na uchumi tegemezi. Hivyo, kubaki katika mduara wa umaskini, hii ndio gharama ya kutokuwa na viwanda. Vijana wanageuzwa kuwa rasilimali watu kwa nchi za Ulaya ,”anasema.

Nini kifanyike? Dk. Magufuli, anayejulikana sio wa ‘kumumunya maneno’ anataka kushughulikiwa vikwazo vinavyochelewesha maendeleo ya sekta ya viwanda ndani ya SADC na Afrika kwa jumla.

Akiwa mzoefu wa muda mrefu kuongoza Wizara ya Ujenzi, anataja maeneo kama uboreshaji miundombinu kupitia kujenga wa barabara zinazounganisha nchi hizo, kwamba yanarahisisha usafirishaji bidhaa wanazozalisha.

“Ndani ya nchi za SADC kuna fursa nyingi za uwekezaji wa viwanda, ikiwamo madini, kilimo, uvuvi, ufugaji, hivyo tuchangamkie soko hili,” anasema.

Pia, aliitahadharisha Sekretarieti ya SADC kujitathmini, akipiga marufuku matumizi ya bajeti kwa semina na kongamano, badala yake ijikite katika maendeleo zaidi. 

Dk. Tax anena

Katika maelezo yake kwa wana SADC waliohudhuria mkutano huo Dk Tax, anabainisha nchi zote zimekuwa zikifanya jitihada kufikia kiwango cha uchumi cha asilimia saba na hadi sasa Tanzania pekee ndio imefikia kigezo hicho. Anataja njia ya mafanikio ni kuwa na uchumi mpana.

Anashauri, viongozi wa nchi za SADC wanajipanga upya kupata ufumbuzi wa pamoja, ikiwamo kuzingatia taratibu za mtangamano (integration) zilizowekwa.

“SADC ilikuwa imejipangia kuwa na uchumi wa zaidi ya asilimia saba lakini nchi nyingi zimefikia asilimia 3.1, hiyo ikiwa chini ya asilimia ya Umoja wa Afika(AU) iliyofikia asilimia tatu,” anasema.

Dk. Tax anataja sababu inayodidimiza SADC, ni kasi yake ya ukuaji uchumi, Afrika Mashariki iko katika wastani wa asilimia 5.7; Afrika Kaskazini, asilimia 4.8; na Afrika Magharibi asilimia 3.3.

Mwenyekiti  msatafu

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Rais Geingob, alibainisha umuhimu wa nchi za SADC kuwashirikisha vijana kuleta maendeleo ya kila nchi.

Kwa kutambua robo tatu ya wananchi wao ni vijana, hakuna sababu ya vijana kwenda nchi za Ulaya kwa ajili ya kutafuta ajira, wakati rasilimali tunazo,” anasema Rais Geingob.

Anashauri ni vyema SADC kuwa na mikakati madhubuti itakayofanikisha vijana kupata nafasi ya kushiriki katika masuala ya uchumi kwa hatua, hivyo kuchochea maendeleo kwa nchi za jumuiya hiyo.

Baraza Biashara

Mwenyekiti wa Baraza la Biashara nchi za SADC, Charity Mwiya, kutoka Namibia, anasema ni muhimu kuwawekea mazingira wezeshi wanawake kibiashara, katika kufikia malengo ya kukuza uchumi kwa nchi za SADC.

“Wanawake wengi ndiyo wapo kwenye biashara na ujasiriamali, hivyo mazingira wezeshi yanafaa kuwekwa ili nchi hizo zifikie malengo.hatuwezi kuzungumzia biashara bila kumtaja mwanamke,” anasema Mwiya.

Habari Kubwa