Wananchi wapiga kura kubaini wezi wa mifugo

06Sep 2019
Allan lsack
MBULU
Nipashe
Wananchi wapiga kura kubaini wezi wa mifugo

WANANCHI wa Bonde la Yaeda Chini, wanaopakana na Wilaya za Mbulu mkoani Manyara na Karatu mkoa wa Arusha, wamepiga kura ya kuwafichua watuhumiwa wa wizi wa wa mifugo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Chelestino Mofuga na Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo, walisimamia kura hizo, ili kukomesha wizi wa mifugo  eneo la mpakani mwa wilaya hizo.

Theresia alisema lengo la kupigwa kwa kura hizo ni kukomesha  wizi kwenye eneo hilo, na kazi hiyo, ilifanyika kwa kuandika majina ya watu wanaodaiwa kuiba mifugo au wanaoshirikiana na wezi.

Mofuga alisema, pia waliwabaini mahalifu walioharibu miundombinu ya alama za mipaka ya bonde hilo na walipiga kura kwa kuandika majina ya wahusika wote.

"Hii ndiyo njia sahihi ya kutafuta wahalifu tunaamini hamtaweza kuandika majina ya watu kwa kuwaonea, na matumaini yangu tabia hii itafikia mwisho, na wizi huu utafikia kikomo maana wahusika wanajulikana na wakiendelea na tabia hii serikali itawashughulikia," alisema.

Mahongo alisema kwa sababu wameteuliwa na kula kiapo kuwa watawatumikia wananchi, hawatakubali kuona wezi wachache wanaharibu amani na kuwasababishia wananchi umaskini.

"Majina haya tutaondoka nayo ili kuyashughulika nyie wenyewe mtaona kwa vitendo na wezi hawa wataacha wizi kwani muda siyo mrefu watabainika.

Awali, baadhi ya wananchi wa eneo hilo, walituhumiana kuibiana mifugo ndipo serikali ikaandaa utaratibu wa kupiga kura za siri kwa kuandika majina ya wahusika wa matukio hayo ili kuwabaini wahalifu.

Mkazi wa Kijiji cha Matala, Julius John, alisema ana amini wezi wa mifugo wanashirikiana na mtandao mkubwa wa watu wanaoishi sehemu hizo, kuiba na kuuza mifugo hiyo.

John alisema haiwezekani mtu kutoka mbali kuiba mifugo kijijini hapo, kama hana mtandao wa watu wanaoshirikiana nao kutenda uhalifu huo.

Habari Kubwa