Wasongamana maabara moja

06Sep 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Wasongamana maabara moja

WANAFUNZI wa Shule ya Sekondari ya Sawe iliyoko Kata ya Masama Mashariki,  Hai mkoani Kilimanjaro, wanarundikana katika chumba kimoja cha maabara kujifunza kwa vitendo masomo ya Fizikia, Baiolojia na Kemia.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo.

Hali hiyo inatajwa kuathiri zaidi upatikanaji wa wanafaunzi waliofanya vizuri katika masomo hayo, hivyo kuendelea kuonyesha alama nyekundu juu ya upatikanaji wa wataalamu wa masomo ya sayansi na walimu wa masomo hayo, hasa kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia na uchumi wa viwanda tunaoutegemea.

Hayo yamo katika taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo, aliyoiwasilisha mbele ya kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika taarifa yake, Sintoo alisema: "Kwa sasa serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba shule hiyo inapata maabara za masomo hayo na kumaliza tatizo hilo."

 

Upungufu wa maabara za sayansi kwenye shule za sekondari katika baadhi ya mikoa nchini umeendelea kuwa changamoto katika ufaulu wa wanafunzi wa masomo hayo.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika mwaka wa fedha 2018/19, serikali ilijenga maabara 165 za masomo ya sayansi katika shule mbalimbali nchini.

Kwa muktadha huo, serikali inataka kila shule inayofundisha masomo ya sayansi kuwa na maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Mwaka 2017 kulikuwa na maabara 2,151 katika shule za sekondari nchini, mahitaji yalikuwa 4,797. Hali hii ilionyesha upungufu wa maabara 2,646. Hata hivyo, wilaya 18 kati ya 184 zilizorodheshwa zilikuwa na upungufu uliozidi asilimia 50.

Habari Kubwa