Vifo vya mama, mtoto sasa tishio

06Sep 2019
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Vifo vya mama, mtoto sasa tishio

TAKWIMU za vifo vya mama na mtoto katika Mkoa wa Mbeya zinaonyesha mwaka 2018 watoto wachanga 500 walifariki wakati wa kuzaliwa, huku kinamama 75 wakipoteza maisha wakati wa kujifungua.

Hayo yalisemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk. Salum Manyatta, wakati wa mafunzo ya matumizi ya dawa za usingizi wakati wa kufanya upasuaji. Mafunzo hayo yalitolewa kwa wataalamu wa afya wa mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Alisema chanzo cha vifo hivyo ni kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za usingizi ambapo alisema takwimu hizo za watoto ni wenye umri wa kuanzia siku sifuri mpaka siku 28.

Alisema mafunzo hayo ya matumizi ya dawa za usingizi yanayotolewa kwa wataalamu yamekuja muda mwafaka kwa maelezo kuwa yatasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.

Dk. Manyatta alisema katika Mkoa wa Mbeya kuna hospitali 25 zinazotoa huduma ya usingizi na kwamba kati ya vituo vya afya 16 ni vituo sita vinavyotoa huduma hiyo.

Aliishauri serikali kuwaacha wataalamu waliopata mafunzo hayo kuendelea kufanya kazi hiyo badala ya kubadilishiwa majukumu kama ambavyo imekuwa ikitokea kwa taaluma zingine.

Mratibu wa mafunzo hayo, Dk. Neimar Yusuph ambaye ni mtaalamu wa usingizi kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga, alisema waliamua kutoa mafunzo hayo baada ya kubaini kuwa kuna changamoto kubwa ya matumizi ya dawa za usingizi.

Alisema walipita katika vituo vingi vya afya pamoja na hospitali na wakabaini kuwa kuna tatizo hilo ambalo linasababisha matatizo ya kiafya hasa kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Baada ya kutoa mafunzo haya tunakusudia kuanza ufuatiliaji ili tupate mrejesho wa kile tunachofundisha ikiwamo kuwafuatilia hawa wataalamu kuona kama kuna mabadiliko ya takwimu za vifo vya mama na mtoto.

Mtaalamu wa dawa za usingizi kutoka katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Rukwa, Dk. Prosper Massawe, alisema katika mkoa wake vifo vya mama na mtoto vimekuwa vikipungua lakini kutokana na mafunzo hayo anaamini vitapungua zaidi.

Alisema watahakikisha wanawafundisha wataalamu wengine kutoa dawa za usingizi kwa usahihi wakati wa kufanya upasuaji wa aina yoyote ili kuwaepusha wagonjwa na hatari ya kupoteza maisha.

Habari Kubwa