Stars: Tutasonga mbele

06Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Stars: Tutasonga mbele
  • ***Yajipanga kufanya makubwa katika mechi ya marudiano Jumapili, lakini...

WAKATI kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), kikirejea nchini jana jioni, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Suleiman Matola, amesema kuwa anaamini watamaliza vema kibarua walichonacho dhidi ya Burundi ambacho walikianza wakiwa ugenini.

Taifa Stars ambayo ililazimisha sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza, inatarajia kurudiana na Burundi Jumapili na mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya mashindano ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kuchezwa mwaka 2022 nchini Qatar.

Akizungumza na gazeti hili jana, Matola, alisema kuwa mechi ya juzi ilikuwa ngumu, lakini wachezaji wa timu hiyo walipambana na kucheza kwa nguvu na hatimaye kufanikiwa kusawazisha.

Matola, Kocha mpya wa Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, alisema kuwa wachezaji wa timu hiyo sasa wameanza kucheza soka "linaloeleweka" na wanaamini baada ya kurejea nyumbani, watajipanga vema ili kuhakikisha wanashinda na kusonga mbele katika mashindano hayo.

"Tunapenda kuwapongeza wachezaji, wameweza kucheza kwa nguvu na maelekezo zaidi, japokuwa kipindi cha pili tulionekana kuchoka, nafikiri ni kutokana na hali ya hewa na uchovu wa safari, tunasema hatutawaangusha, kutokana tunarudi nyumbani, tutajipanga na tutafanya kile kitu ambacho kila Mtanzania anakihitaji, nina imani tutasonga mbele," alisema Matola.

Kocha huyo aliongeza kuwa bado Stars inahitaji kupewa ushirikiano na wadau wote na kwa kufanya hivyo, anaamini wataendelea kupeperusha vema bendera ya Tanzania kwa kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta, alisema kuwa ilikuwa ni mechi ngumu na yenye ushindani, lakini matokeo ya sare waliyopata, yatawasaidia kujipanga upya kuelekea mchezo wa marudiano.

"Kwanza nina furaha kwa jitihada ambazo zimeonyeshwa na wachezaji wenzangu, tumejitahidi kwa pamoja na kupata matokeo ambayo yatatusaidia kwa ajili ya mchezo ujao, mechi ya kwanza imeisha, tumepata sare, tunaenda nyumbani, tunaamini Watanzania watajitokeza kutushangilia ili kutufanya tusonge katika raundi inayofuata," Samatta alisema.

Naye kipa Juma Kaseja, alisema kuwa mshikamano na umoja unahitajika zaidi ili Taifa Stars iweze kufanya vema katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.

"Sare ya 1-1 ni faida kwetu, tushikamane, kila siku mimi ninasema, Tanzania ni ya kwetu, timu ni yetu, mechi ya marudiano itakuwa ngumu zaidi ya leo, tushikamane ili tuweze kutinga hatua ya makundi," Kaseja, ambaye amerejeshwa katika kikosi hicho na Kaimu Kocha Mkuu, Etienne Ndayiragije alisema.

Burundi ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao katika mchezo huo kupitia kwa Amissi Cedric na Simon Msuva aliisawazishia Stars na kuamsha furaha ya Watanzania wote waliokuwa wanaufuatilia mchezo huo.