Simba yajipanga kulinda heshima

06Sep 2019
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba yajipanga kulinda heshima

MAWINDONI! Kikosi cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, kimeanza maandalizi ya kuwakaribisha Mtibwa Sugar katika mechi ya ligi hiyo inayotarajiwa kuchezwa Septemba 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, aliliambia gazeti hili kwamba wameanza programu maalumu ambayo itawaimarisha wachezaji wao na kuwa tayari kuendelea na mbio za kutetea taji hilo wanalolishikilia msimu wa pili mfululizo.

Rweyemamu alisema kuwa anaamini mara baada ya nyota wao walioko kwenye timu za Taifa mbalimbali kurejea, watakamilisha baadhi ya mbinu muhimu ambazo zitawafanya kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kushinda kila mchezo watakaocheza.

"Mikakati ya kocha wetu (Patrick Aussems), ni kuhakikisha hatupotezi mchezo hata mmoja katika Ligi Kuu msimu huu na kulinda heshima, lengo letu ni kutetea taji mapema, leo (jana) tunatarajia kupeana programu kamili baada ya kuanza mazoezi upya baada ya mapumziko mafupi," alisema meneja huyo.

Aliongeza kuwa baada ya kutolewa mapema katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, nguvu zao zote zinaitazama Ligi Kuu Bara, hivyo wanahitaji kuona wanawapa furaha mashabiki na wanachama wao.

Baada ya kucheza na Mtibwa Sugar, mabingwa hao watetezi wataendelea kubakia jijini Dar es Salaam kwa kuwasubiri Lipuli FC, mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaochezwa Septemba 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru.

Habari Kubwa