Bodaboda sasa wajifunze, wafuate sheria barabarani

06Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bodaboda sasa wajifunze, wafuate sheria barabarani

UKAIDI unaofanywa na waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, ni kero kwa wananchi wengi kwa sababu unawasababishia usumbufu, zikiwamo ajali zisizo kuwa na ulazima.

Usumbufu huo hauwapati wananchi pekee, bali hata mamlaka za serikali, kikiwamo Kikosi cha Usalama Barabarani hususan wanapowatoza faini kutokana na makosa mbalimbali.

Kutokana na tatizo hili sugu, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini,  Fortunatus Musilim, amewataka askari wa usalama barabarani kuwakamata madereva wa bodaboda wanaokiuka sheria za usalama barabarani na kuwachukulia hatua kama ilivyo kwa madereva wengine.

Aliwataka madereva hao wanaodaiwa faini za muda mrefu kulipa mara moja kuepuka misukosuko barabarani.

Alisema dereva wa bodaboda akikamatwa mmiliki ataitwa ili kuchukua pikipiki na dereva atafikishwa mahakamani ili kuondoa mrundikano wa vyombo hivyo katika vituo vya polisi.

Alisema anaamini kuwa hakuna mmiliki ambaye anapenda kuona dereva wake wa bodaboda anavunja sheria barabarani, na kuwa ikitokea mmiliki ataitwa kuchukua pikipiki, lakini dereva ataendelea kushikiliwa na kumfikisha mahakamani.

Aliongeza kuwa wanachotaka ni pikipiki zote kuchukuliwa na kuondolewa kwenye vituo vya polisi, baada ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani ili kuondoa mrundikano katika vituo hivyo.

Mkuu huyo wa trafiki ametoa onyo hilo kutokana na mwenendo mbovu wa madereva wa bodaboda katika maeneo mengi ya nchi kukiuka sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani kwa makusudi.

Tunasema kuwa wanafanya hivyo makusudi kwa kuwa wamekuwa wakipewa maelekezo, elimu na hata kuonywa, lakini wanapuuza badala yake kuendesha pikipiki zao kama wanavyotaka wao.

Kwa mfano, wamekuwa wakisisitizwa kuvaa kofia ngumu kila wakati kwa ajili ya usalama wao hususani pale zinapotokea ajali, lakini wanakaidi kuzivaa, hivyo mara kwa mara kukamatwa na askari na kuwatoza faini.

Makosa mengine ni kupita katika maeneo ambayo wanapaswa kusimama kusubiri waruhusiwe na taa za kuongoza magari, lakini hawasimami, hivyo wakati mwingine kusababisha ajali.

Bodaboda wanatakiwa kuvaa viatu, lakini wengi wao wanakiuka badala yake kuvaa ndala au viatu vya wazi, hivyo kujikuta mara kwa mara wakiandikiwa kulipa faini, ambazo huwa wagumu kuzilipa.

Matokeo yake pikipiki zao hukaa muda mrefu katika vituo vya polisi na kusababisha mrundikano.

Hali hiyo huwasababishia usumbufu mkubwa wamiliki wa pikipiki hizo kutokana na kutakiwa kwenda kuzikomboa katika vituo vya polisi, hivyo tunapendekeza kuwa kuna haja ya kuangaliwa upya biashara ya usafirishaji abiria kwa kutumia bodaboda na ikiwezekana itungwe sheria mahususi.

Sheria hiyo iwalazimishe madereva wa bodaboda kuhudhuria mafunzo katika taasisi zinazotambuliwa na serikali ili wawe na ujuzi pamoja na kuzijua sheria za usalama barabarani, badala ya mhusika kujifunzia vichochoroni chombo hicho siku moja kisha anaanza kuendesha kwenye barabara kuu!

Kwa kufanya hivyo, vitendo vya kihuni, ubabe vitapungua kwenye barabara zetu pamoja na ajali za kizembe.

Habari Kubwa