Salamba apata ulaji mpya Misri

06Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Salamba apata ulaji mpya Misri

MSHAMBULIAJI wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Adam Salamba, amepata mkataba wa kujiunga na klabu ya Al Jahra ya Misri, imefahamika.

Salamba ambaye alitua Simba akitokea Lipuli FC ya mkoani Iringa, alikuwa amepelekwa Namungo FC ya Ruangwa Lindi kwa mkopo.

Taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa, Simba inatarajia kulipwa kitita cha Sh. milioni 100 kwa ajili ya kumuuza mshambuliaji huyo ambaye anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano na klabu hiyo.

Chanzo chetu kinasema kuwa, mshambuliaji huyo pia anatarajiwa kulipwa mshahara wa Sh. milioni 9.5 katika mkataba wake mpya na klabu hiyo.

"Mafanikio huja kutokana na kupambana na kutokata tamaa, Mungu mkubwa," alisema Salamba baada ya kufanikisha mazungumzo ya kujiunga na Al Jahra.

Mshambuliaji huyo hakuwa na namba katika kikosi cha kwanza cha Simba na hivyo kusababisha kutolewa kwa mkopo ili kwenda kuimarisha kiwango chake.

Habari Kubwa