Songas yaipa serikali gawio la bil. 8.8/-

06Sep 2019
Moshi Lusonzo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Songas yaipa serikali gawio la bil. 8.8/-

KAMPUNI ya kuchakata umeme kutokana na nishati ya gesi ya Songas imetoa gawio la Sh. bilioni 8.8 kwa serikali inayotokana na faida.

Mkurugenzi Mtendaji wa Songas, Nigel Whittaker

Akizungumza jijini Dar es salaam jana wakati akikabidhi gawio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Songas, Nigel Whittaker, amesema kiasi hicho kinatokana na hisa ilizonazo kupitia Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na  Shirika la Taifa la Maendeleo ya Petroli (TPDC).

 Alisema kiasi hicho kinatokana na uwiano wa hisa ndani ya kampuni, Tanesco imepata gawio la Sh. bilioni 2.2 na TPDC imepokea Sh. bilioni 6.6.

“Serikali kama mwanahisa wa kampuni kupitia mashirika yake tumeamua kulipa kiasi hicho kama gawio la faida kwa mujibu wa sheria na sisi kama kampuni tunajivunia kutokana na tukio hili muhimu,” alisema Whittaker.

Alisema Songas hadi sasa inaongoza kwa uzalishaji wa umeme wa gesi Afrika Mashariki kwa asilimia 20 kwamba  mikakati inaendelea kuongeza uzalishaji kutoka megwati 180 mwaka 2012 hadi kufikia 250.

“Tunaipongeza serikali kwa juhudi zake za kuhakikisha nishati ya umeme inazidi kuongezeka na kusababisha kupata matokeo chanya katika uchumi wa viwanda. Songas tutazidi kuchangia juhudi hizi kwa kuongeza uzalishaji maradufu,” alisema.

Ofisa Mkuu wa Fedha, Anael Samuel, alisema Songas itazidi kutoa gawio kwa wanahisa wake kila mwaka na kwamba serikali inanufaika kutokana na uwekezaji katika kampuni hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya serikali, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa TPDC, Godwin Kailembo, aliishukuru kampuni hiyo kwa kutoa fedha hizo ambazo zitatumika kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Aliipongeza kampuni hiyo kwa kutoa fedha hizo ambazo zitaelekezwa kutatua kero za wananchi maskini.

Habari Kubwa