Magari 54 ya mtu mmoja kunadiwa Dar

06Sep 2019
Joseph Mwendapole
Nipashe
Magari 54 ya mtu mmoja kunadiwa Dar

JINAMIZI la nyumba kuuzwa kutokana na wamiliki kushindwa kurejesha mikopo sasa limehamia kwa mtu mmoja anayemiliki magari 54 aina ya IST, ambayo yanauzwa kesho baada ya kushindwa kurejesha mkopo.

Mmiliki wa magari hayo anadaiwa kukopa benki ya ICB na kununua magari hayo kwa ajili ya kuyafanyia biashara, lakini muda ulipopita bila kukamilisha mkopo huo, benki hiyo iliamua kuyakamata na kuamuru yauzwe kufidia mkopo huo.

Benki hiyo ilitoa zabuni kwa kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart kuendesha mnada wa kuuza magari hayo kesho Jumamosi, maeneo ya Bahari  Beach jijini Dar es Salaam kuanzia asubuhi hadi jioni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Yono, Scholastica Kevela, alisema wameweka masharti makali ya kuingia kwenye mnada huo ili kuwaepuka watu aina ya Dk. Shika, ambao huingia kwenye minada hiyo kwa ajili ya kuivuruga.

“Safari hii tumejipanga sawa sawa tumeweka utaratibu mzuri kuhakikisha kwamba hakutakuwa na watu wa aina ya Dk. Shika kwa sababu utapoingia kwenye mnada utatakiwa kuacha getini Sh. 2,000,000 tunaweka kama dhamana ukiharibu mnada hatutakurudishia na kama hutaharibu mnada unarudishiwa,” alisema Scholastica.

Alisema tangu kutangazwa kwa mnada huo mamia ya watu wamekuwa wakifurika kwenye yadi ya Yono Bahari Beach kwa ajili ya kukagua magari hayo ambayo mmiliki wake alikuwa akiyatumia kibiashara kwa usafiri wa mitandanoni.

Mbali na IST hizo, alisema kwenye mnada huo watauza magari mengine ya aina mbalimbali ambayo yamekamatwa kutokana na makosa mbalimbali yakiwamo ya ukwepaji wa kodi.

Habari Kubwa