Wanavijiji 80,000 Mugango kunywa maji ya Ziwa Victoria

07Sep 2019
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanavijiji 80,000 Mugango kunywa maji ya Ziwa Victoria

SERIKALI imepanga kumfikishia kila Mtanzania maji safi na salama bila kujali eneo analoishi. Mpango huo unawafikia walioko vijijini kwa kuwapa huduma hiyo kwa asilimia 85.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo (kulia waliokaa), akisaini mkataba na mmoja wa wawakilishi wa kampuni inayojenga mradi wa bomba kubwa la maji kutoka Mugango, Musoma Vijijini, kupitia Kiabakari hadi Butiama, huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima

Ikimaanisha kuwa kwa kila watu 100 wanaoishi vijijini takribani wananchi 85 watakuwa wanapata maji ya bomba kwa namna yeyote ile na kwa gharama nafuu.

Kwa wakazi wa mijini asilimia 95 itakuwa inapata huduma hiyo, kwa tafsiri hiyo ni kama kila mtu anayeishi mjini atapata huduma  ya maji safi na salama.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makama Mbarawa, anasema serikali inataka kuwafikishia maji kwa  asilimia 95 walioko mijini na asilimia 85 wakazi wa vijijini.

Kutokana na uamuzi huo wa serikali, miradi mbalimbali ya maji inaendelea kutekelezwa na mingine kusainiwa kwa ajili ya utekelezaji ili wananchi waweze kunufaika na huduma hiyo muhimu.

Mradi wa bomba la maji safi na salama kutoka ziwa Victoria eneo la Mugango, Musoma Vijijini kupitia Kiabakari hadi wilayani Butiama mkoani Mara ni miongoni mwa miradi hiyo inayotekelezwa kutimiza azma hiyo.

Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Kiarabu kwa Maendeleo ya Afrika (BADEA) na Mfuko wa Maendeleo wa Saudia (SFD) zimeingia mkataba wa utekelezaji wa mradi huo.

Ujenzi wa huduma hiyo unaogharimu Sh. bilioni 70, unatarajia kuanza wakati wowote baada ya mkataba kutiwa saini tangu Agosti mwaka huu kazi iliyofanyika Nyamisisi wilayani Butiama.

Serikali iliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, huku Mkoa uliongozwa na Mkuu wa Mkoa, Adam Malima, kwenye hafla hiyo ya utiaji saini.

Wengine wanaoshuhudia tukio hilo lililofanyika Agosti 15 mwaka huu ni wakuu wa wilaya za Musoma na Butiama, wakurugenzi wa halmashauri za wilaya hizo.

Mbali na hao walikuwapo pia wabunge Profesa  Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini), Agnes Marwa na Amina Makilagi (viti maalum), madiwani na viongozi wa chama na serikali.

Dokta Vincent Anney, ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, ambako bomba hilo linaanzia kwenye Kijiji cha Kwibara kilichoko kata ya Mugango, kuelekea maeneo mengine.

WATAKAONUFAIKA

Anney anasema mbali na wakazi wa kata ya Mugango, ambako bomba hilo linaanzia, wananchi  wengine 80,000 waliopo kwenye vijiji 13 eneo ambalo bomba hilo litapita, wanatarajia kunufaika na mradi huo.

Mkuu huyo wa wilaya anasema mradi huo mkongwe ni wa siku nyingi tangu mwaka 1974 na kwamba serikali imetenga Sh. bilioni 8.5 ili wakazi Musoma Vijijini na wa Butiama wanufaike na huduma hiyo muhimu.

Dokta Anney anasema, mradi huo unatarajia kukamilika ndani ya miezi 24 na kwamba mbali na huo, kuna mingine inayoendelea wilayani mwake na hasa kwenye wilaya ya Musoma Vijijini.

"Kuna mradi wa maziwa makuu, ambao vijiji vyote 33 vya Musoma Vijijini vilivyoko karibu na Ziwa Victoria vimo kwenye mradi huo na usanifu umeshafanyika," anasema Mkuu wa Wilaya.

Anasema serikali inajipanga kwa utekelezaji na pia maji yanayozalishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa), kwa ajili ya Mji wa Musoma ni mengi ikiwa ni takriban asilimia 50 ya maji yanayozalishwa, hivyo yatasambazwa vijijini.

Anasema mradi huo ni wa kipekee kwa kuwa maji yanayozalishwa yana uwezo wa kuchotwa na kunywewa kutoka bombani bila ya kuchemshwa kutokana na kuchujwa na kuwekwa dawa ya kutosha ya kutibu maji.

"Serikali imeamua vijijini vya Musoma Vijijini na Butiama visambaziwe maji hayo ya ziada, ambapo vijiji vya Musoma Vijijini ni vya kata za Etaro, Nyegina, Nyakatende na Ifulifu," anasema.

Anasema utekelezaji wa mradi huo umeanza na pia anataja mingine inayotekelezwa kuwa ni ya vijiji vya Bujaga, Bulinga, Bukima, Kwikerege,  Chitare, Makojo, Suguti, Kusenyi, Chirorwe hadi Wanyere.

"Tangi lenye uwezo wa kuchukua lita 225,000, limejengwa kijiji cha Bujaga, vituo 18 vya kuchotea maji, vioski viwili vya kuuzia maji, birika la kunyweshea mifugo na utandazaji wa mabomba ya kusambazia maji," anasema Anney.

Mkuu huyo wa wilaya anasema serikali imedhamiria kumaliza tatizo la ukosefu wa maji safi na salama, na kuwataka wananchi waendelee kuiunga mkono kwa kazi ambazo inafanya kwa ajili yao.

Anafafanua kuwa kuna miradi mingine ambayo usanifu wake umekamilika ambayo ni ya vijiji vya kata za Bugoji, Nyambono, Bugwema, Musanja na Nyamrandirira, na kwamba maombi ya fedha za utekelezaji wa usambazaji wa maji yamefikishwa kwenye serikali kuu.

WANANCHI

Kwa niaba ya wananchi wa vijiji 68 vya Musoma Vijijini, mbunge wao Profesa Sospeter Muhongo, anatoa shukrani za dhati kwa Serikali yao kwa kuanza kutekeleza miradi ya usambazaji maji safi na salama vijijini mwao.

"Shukrani maalum ni kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, kwa kuanza kutimiza ahadi yake ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la maji la Mugango-Kiabakari-Butiama," Prof. Muhongo anasema.

Anasema wananchi wa Musoma Vijijini sasa wanakaribia kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama, ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo kwa muda mrefu.

"Wananchi hutembea umbali mrefu kufuata huduma ya maji pembezoni mwa ziwa Victoria na wengine walio mbali na ziwa hulazimika kuyatafuta kwenye visima vya kienyeji, lakini sasa wataondokana na hali hiyo," anasema.

Mbunge huyo anasema kilio cha wananchi kimewafikia viongozi wa serikali moja kwa moja, na sasa miradi ya maji inatekelezwa ili kuwaondolea changamoto hiyo ya ukosefu wa maji.

"Kwa mfano vijiji vyote 33 vya Musoma Vijijini vilivyoko karibu na ziwa Victoria kuwekwa kwenye mradi wa maziwa makuu ni hatua nzuri sana ndio maana wananchi wanatoa shukrani kwa serikali yao," anasema.

Prof. Muhongo anasema jimbo lake lina jumla ya vijiji 68, na kwamba 33 kati hivyo viko kwenye mradi huo wa maziwa makuu na vilivyosalia vinaendelea kufanyiwa mchakato wa kupata huduma ya maji safi na salama.

Habari Kubwa