Waziri Mahiga amwagia sifa Makonda

07Sep 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Waziri Mahiga amwagia sifa Makonda

WIZARA ya Katiba na Sheria imeitaka mikoa mbalimbali nchini kuiga mfano wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wa kuweka jitihada ya kufuatilia masuala ya kijamii yanayogusa maisha ya watu.

Balozi Augastine Mahiga

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri mwenye dhamana Balozi Augastine Mahiga, wakati akipokea mapendekezo ya maboresho ya Sheria ya Mirathi na Ndoa inayowakandamiza wanawake.

Balozi Mahiga alisema, Mkoa wa Dar es Salaam unapaswa kuigwa na mikoa mingine kwa sababu umeisaidia wizara kujua nini kinatendeka katika mikoa kwa upande wa kinamama wajane.

"Ninaomba mikoa yote igeni Dar es Salaam kwa sababu amekusanya maoni ambayo ni mwongozo katika mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya mirathi na ndoa," alisema Mahiga.

Alisema kuna manyanyaso mengi vijijini na mijini, lakini waathirika wanakosa mwongozo wa kufikisha sehemu husika.

"Naomba mikoa mingine mikubwa igeni mfano wa Makonda, lengo ni kuboresha sheria hiyo ili isiwakandamize," alisema Balozi Mahiga.

Hata hivyo, alisema wanatarajia kuwasilisha hoja hiyo bungeni wiki hii kama taarifa ili ijadiliwe na baadaye kupitishwa kama itakubalika.

Aliwataka Watanzania kujua maana ya ulinzi jamii, jinsi ya kuongeza thamani katika maisha ya kila siku.

"Naomba wanahabari mtusaidie kutangaza kwa sababu social security (ulinzi jamii) wengi hawajui, lakini ipo duniani na inalinda maisha ya binadamu," alisema Balozi Mahiga.

Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Makonda, alisema kinamama wengi wananyanyasika ndio maana katika mkoa wake kwa kushirikiana na watendaji wake walifanyia kazi suala la sheria ya maboresho ya mirathi na ndoa.

Alisema wana kila sababu ya kufanya hivyo kwa sababu sheria hiyo ni ya muda mrefu na imepitwa na wakati.

Alisema mapendekezo yao ambayo yamewasilishwa kwa Waziri Mahiga wanaimani yatafanyiwa kazi kwa sababu yamefikia sehemu husika.

Habari Kubwa