Bunge latoa angalizo usajili alama za vidole

07Sep 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Bunge latoa angalizo usajili alama za vidole

BUNGE limeitaka serikali kuweka katazo kwa kampuni za simu na mawakala wao kutouza wala kuunganisha kadi za simu ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole.

Limesema hatua hiyo itawaondolea wananchi mzigo wa adhabu watakaoupata pindi watakapotumia kadi za simu ambazo hazijasajiliwa kwenye mfumo huo licha ya kununua kadi hizo kihalali.

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mjumbe wa Kamati hiyo, Asha Abdallah Juma, alisema serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya kutumia laini za simu zisizosajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole.

“Serikali ijikite zaidi kwenye teknolojia ya kuzima simu zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa kwa Mfumo wa Biometria (alama za vidole) baada ya muda utakaokuwa umetolewa,” alisema.

Asha alieleza hatua hiyo ni muhimu badala ya kujikita kwenye adhabu kali ambazo zinaweza kukosa uhalisia kwa wananchi wa kawaida ambao ndiyo watumiaji wa simu.

Mbunge huyo wa Viti Maalum (CCM), alibainisha kuwa kihalisia makosa hayo ni ya kampuni za simu za mikononi na mawakala wao ambazo wanauza kadi za simu bila kuhakikisha zimesajiliwa kwenye mfumo wa alama za vidole.

Vilevile, alisema serikali inapaswa kuhakikisha mfumo wa utoaji vitambulisho vya taifa unarahisishwa kwa kuwafikia wananchi wote.

Awali, akiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta, Sura ya 309, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prof. Aderaldus Kilangi, alisema marekebisho hayo ni muhimu kwa maslahi ya umma.

Alisema yana lengo la kuimarisha udhibiti wa matumizi ya huduma za mawasiliano ya kieletroniki na kudhibiti watumiaji wenye lengo la kurubuni wananchi kwa kutumia kadi za simu zisizosajiliwa kwa majina tofauti.

“Pia yanalenga kuimarisha usalama wa watumiaji wa huduma za kimtandao ili kupunguza wimbi la uhalifu na kuhuisha sheria kuendana na hali ya sasa ya usajili wa laini za simu kwa alama za vidole,” alisema.

Akiwasilisha maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni kuhusu marekebisho hayo, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Latifah Chande, alisema kambi hiyo inaona ni jukumu la kampuni za simu kuhakikisha laini ya simu ambayo haijasajiliwa haifanyi kazi.

"Endapo kutakuwa na laini ambazo hazijasajiliwa zinafanya kazi basi kosa hilo litakuwa la kampuni ya simu na siyo kosa la mtumiaji wa huduma hizo," alisema.

Habari Kubwa