Kila na kheri Stars, tuwachape Burundi

07Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kila na kheri Stars, tuwachape Burundi

KWA mara nyingine kikosi cha Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kinatarajia kushuka dimbani kuwakabili wapinzani wao Burundi katika mechi ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia zinazotarajiwa kufanyika Qatar mwaka 2022.

Mechi hiyo kati ya Stars dhidi ya Burundi, itachezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya Jumatano kutoka sare ya bao 1-1 mjini Bujumbura.

Ili kuwa kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo, Taifa Stars inayofundishwa na Etienne Ndayiragije, raia wa Burundi, inahitaji ushindi wa aina yoyote kwa sababu sare ya kuanzia magoli 2-2 itakuwa imewaondoka kwenye michuano hiyo.

Ni mechi ambazo zinachezwa ndani ya muda mfupi, lakini ni kalenda ambayo imetolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambayo inazihusu timu za mataifa yote.

Stars inatakiwa kujiandaa vema kuhakikisha inashinda mechi hiyo na kuondoa akilini mwao kwamba ina faida ya bao moja la ugenini ambalo walilipata katika mchezo wa kwanza.

Kama wao waliweza kupata goli hilo, wapinzani wao Burundi pia wanaweza kupata bao, kikubwa ni kujilinda na kutumia vizuri nafasi za kufunga watakazozitengeneza katika mchezo huo na hatimaye kuwapa furaha Watanzania.

Nipashe inaamini kuwa endapo wachezaji watakapopata nafasi ya kucheza mechi hiyo watajituma na kupeperusha vema bendera ya Tanzania, hakuna kitakachoshindikana.

Ni wazi kuwa dunia ya leo, mgeni anaweza kupata ushindi, kamwe jambo hili Watanzania tusilikubali, tushikamane, tutapambane kuona Stars inatinga hatua ya makundi na baadaye kutimiza ndoto za kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza.

Pamoja na Tanzania kutuchukua miaka 39 kurejea katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), hicho si kigezo cha kuchukua tena muda mrefu ili kukata tiketi ya kushiriki mashindano hayo makubwa, tunawaamini wachezaji wetu wanaweza kupambana na hatimaye kupata matokeo chanya katika mchezo huo ambao utachezwa kuanzia saa 10:00 jioni.

Kufanya vema kwa Stars, mbali na kutangaza jina la nchi katika ngazi ya kimataifa, pia kutatoa nafasi kwa wachezaji wa Tanzania kunadi vipaji vyao na hatimaye kupata idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa.

Gazeti hili lina imani na kikosi cha Stars pamoja na benchi lake la ufundi, lakini ili waweze kukamilisha kazi yao, mchezaji namba 12 (shabiki) ambaye ni muhimu zaidi, naye anatakiwa kutimiza wajibu wake katika kuhakikisha taifa linaibuka na ushindi kwenye vita hii.

Hata hivyo, Nipashe linawakumbusha wachezaji wa Stars kucheza kwa tahadhari katika mechi hiyo ya marudiano, huku ikikumbuka Burundi ni moja ya timu zilizoonekana kuonyesha soka la kueleweka kwenye fainali za AFCON, licha ya kutolewa kwenye hatua ya makundi.

Mashabiki watakapofika kwa wingi uwanjani kwa lengo la kuwashangilia wachezaji wao kwa dakika zote 90, naamini kila mmoja ataona kuwa ana deni la kupambana kwa lengo la kupata matokeo chanya na si kitu kingine.

Nipashe linapenda pia kuwakumbusha mashambiki wa soka wa hapa nchini, kuwa watulivu kabla ya baada ya mchezo huo kumalizika na kuendeleza sifa yetu kuwa Tanzania si sehemu tulivu na ya amani, licha ya kuwapo kwa taarifa za kiongozi mmoja wa Stars na mwandishi wa habari (majina tunayahifadhi) kufanyiwa vurugu za hapa na pale kule mjini Bujumbura.

Kwa nguvu ile ile iliyotumika kuwaondoka Kenya (Harambee Stars) katika safari ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), itumike pia kuwafunga Burundi na hatimaye kusonga mbele.

Kila na kheri Taifa Stars, Mungu ibariki Tanzania.

Habari Kubwa