Ya Simba na KMC yasijitokeze kesho

07Sep 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ya Simba na KMC yasijitokeze kesho

TIMU ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), kesho itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya wenzao kutoka Burundi katika mechi ya marudiano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022 nchini Qatar.

Kwenye mechi ya kwanza iliyocheza mjini Bujumbura nchini Burundi, Stars ililazimisha sare ya bao 1-1.

Ili kutinga katika hatua ya makundi, Taifa Stars inatakiwa kutoka sare isiyo na magoli, au ushindi wa idadi yoyote ile ya magoli.

Sare ya kuanzia magoli 2-2 na kuendelea au kufungwa idadi yoyote ya magoli itaitoa Stars kwenye kinyang'anyiro cha mashindano hayo.

Kinachonifanya niandike hili, ni wasiwasi wangu ambao ulianza kuniingia tangu kwenye mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya KMC dhidi ya AS Kigali na mechi nyingine ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa kati ya Simba dhidi ya UD Songo.

Baada ya kutoka sare ya bila kufungana ugenini, KMC ilionekana ina nafasi kubwa ya kushinda mechi kwani inacheza ugenini, lakini kilichotokea hakuna aliyeamini, kwani ilichapwa hapa hapa mabao 2-0 na kutolewa kwenye michuano hiyo.

Simba nayo, baada ya sare ya bila kufungana ugenini, ilishangazwa nyumbani ilipolazimishwa sare ya bao 1-1 na kwa matokeo hayo, ikawa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bao la ugenini.

Matokeo haya yawe ni somo kuelekea kwenye mechi ya kesho kwa viongozi, makocha na wachezaji wetu wa Taifa Stars.

Hawatakiwi kubweteka kabisa kuona kama kazi imeisha kwani Burundi wanaweza kupindua matokeo kama zilivyofanya timu nilizozitaja.

Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa Simba na KMC zilitolewa kwa sababu za kisaikolojia zaidi kwani viongozi, makocha na wachezaji wao waliona kama vile wamemaliza kazi na kujiingiza kwenye raundi inayofuata kabla mechi za marudiano hazijachezwa.

Wachezaji wa Taifa Stars inapaswa wakumbushwe kuwa pamoja na sare ya bao 1-1, huku mkononi wakiwa na goli la ugenini, waondokane kabisa na fikra za mechi ile, iwe kama vile haijachezwa na wanachohitaji ni kupambana na kutoka na ushindi tu ili waweze kusonga mbele na si vinginevyo.

Kama akili za wachezaji zikiwa ni kutafuta sare ya bila kufungana kwa bahati mbaya Burundi ikapata bao la mapema, linaweza kabisa kuwachanganya wachezaji na mechi ikaishia hapo.

Nilimsikia Kocha Mkuu wa Burundi akisema kuwa hana wasiwasi na mechi hiyo kwani Stars itacheza kwa kufunguka, tofauti na ilivyocheza Burundi ambapo ilikuwa inazuia zaidi.

"Wao watafunguka, watacheza mpira, hivyo uwanja utakuwa mpana, hapo sisi ndipo tutatumia mwanya huo, lakini pia tutasaka bao la mapema ili kuwapa presha wapinzani wetu." Alisema kocha huyo.

Hiyo ndiyo mbinu watakayoingia nayo, hivyo Stars itabidi ijipange vizuri ili yenyewe ndiyo ianze kushambulia tangu mwanzo ili kupata bao la mapema na kutoruhusu Burundi kumiliki mpira dakika za mwanzo, kwani kitendo hicho kinaweza kusababisha kutimiza lengo lao na kuwatoa mchezoni wachezaji na mashabiki kwa ujumla.

Kila la kheri Taifa Stars, Mungu Ibariki Tanzania kuelekea Qatar mwaka 2022.

Habari Kubwa