Nembo ya mdhamini, TFF isionyeshe udhaifu Yanga

09Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nembo ya mdhamini, TFF isionyeshe udhaifu Yanga

BAADA ya msimu uliopita Ligi Kuu Tanzania Bara kushuhudiwa ikimalizika bila mdhamini mkuu, hatimaye Shirikisho la Soka nchini (TFF), mwezi uliopita liliingia mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya Vodacom kudhamini ligi hiyo kwa Sh. bilioni tisa.

Kupatikana kwa mdhamini mkuu kunakwenda kutatua changamoto kubwa za fedha za usafiri na kwa kiasi fulani uchumi wa klabu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu nchini.

Tulishuhudia timu nyingi msimu uliopita zikilazimika kutembeza bakuli kuchangishana ili kuweza kujiendesha huku kwa TFF hususan kitengo chake cha masoko kikitupiwa lawama kwa kushindwa kutafuta wadhamini.

Hata klabu kongwe kama Yanga, licha ya kuwa na udhamini kutoka Kampuni ya SportPesa bado ililazimika kutembeza bakuli kutokana na gharama za kujiendesha kuwa kubwa.

Hivyo, hatua ya Kampuni ya Vodacom kurejea kwa mara nyingine kudhamini Ligi Kuu ni suala la kupongezwa na kushukuriwa lakini pia kuthaminiwa na kuheshimiwa kwa mkataba huo kwa TFF na wanachama wake ambao ni klabu.

Tulishudia mwaka 2011 wakati TFF ikiwa chini ya uongozi wa Jamal Malinzi, Klabu ya Yanga ikigomea jezi zake kuwa na nembo nyekundu za mdhamini mkuu, Kampuni ya Vodacom kwa kile walichodai kuwa rangi hiyo si utamaduni wao.

TFF wakati huo ililazimika kurudi kuzungumza na Vodacom ambayo iliikubalia Yanga kubadili rangi ya nembo ya mdhamini kutoka nyekundu na nyeupe kuwa kijani.

Hata hivyo, wakati TFF ikitia saini mkataba huo na Vodacom mwezi uliopita, waandishi wa habari walimtaka Rais wa TFF, Wallace Karia, kujua msimamo wa shirikisho hilo kipindi hiki katika suala zima la kuheshimu mkataba huo.

Karia aliweka wazi kwamba katu hawatakubali kuona nembo hiyo ya mdhamini ikichezewa na klabu yoyote itakayofanya hivyo, itakuwa si mwanafamilia wa TFF.

Kwa hakika tunaunga mkono kwa asilimia 100 kauli hiyo ya TFF, kwani kwa ukongwe wetu kama wadau wa soka, ni Ligi Kuu Tanzania Bara tu ndiyo tumeshuhudia klabu ikikataa rangi ya nembo ya mdhamini eti kwa sababu haiendani na rangi ya jezi zao.

Tunachojiuliza kama klabu zote 20 zinazoshiriki ligi hiyo kila moja ikihitaji rangi yake, thamani ya mdhamini itakuwa ni ipi? Ama Yanga ikitumia nembo hiyo nyekundu itapungukiwa na nini?

Umefika wakati kwa Yanga kutambua haipo juu ya kanuni za TFF na tunaamini yapo mambo mengi ya msingi ya kupigania kwa maendeleo ya klabu kuliko kupoteza muda katika hili.

Hatutegemei kuona TFF ikikubali kugeuzwa dhaifu katika hili, aidha tunaona badala ya shirikisho hilo kupoteza muda kwenda kuiomba Vodacom kuiruhusu Yanga kubadili rangi ya nembo, itumie muda huo kuomba klabu hiyo isiwe sehemu ya wanufaika wa udhamini huo.

Lakini pia tunaamini Yanga inaongozwa na wasomi, hivyo watalifikiria kwa mapana zaidi na kutazama kwingineko duniani namna ilivyo kwenye ligi za wenzetu waliopiga hatua kisoka na kuridhia kutumia rangi ya nembo ya mdhamini kama ilivyo badala ya kuendeleza malumbano katika hilo.

Lengo letu ni kuona Ligi Kuu Bara ikivutia kampuni nyingi zaidi kuidhamini ili kuongeza ushindani, lakini kama TFF itakubali kuwa dhaifu katika hili, hakika itakuwa chanzo cha kukimbiza wadhamini.

Habari Kubwa