Wanaume kuingi vyoo vya kike Taifa ni kuwakimbiza viwanjani

09Sep 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanaume kuingi vyoo vya kike Taifa ni kuwakimbiza viwanjani

MWANZONI niliona kama ni bahati mbaya. Lakini nilipokuwa nakwenda kwenye mechi mbalimbali Uwanja wa Taifa niliona hali hiyo ikijitokeza tena na tena.

Nilichokuwa nikikishuhudia huwezi kukiona hata kwenye baa za mitaani. Ni kwamba wanaume wanalazimika kuingia kwenye vyoo vya kike. Hii inawapa tabu sana watoto wa kike wanaokuwa uwanjani.

Waliokuwa tayari ndani wanajikuta wakiwa kwenye vyoo pamoja na wanaume. Wale walio nje wakiona midume inaingia, hawaingii tena. Sasa sijajua huwa wanakwenda kujisaidia wapi.

Hii ndiyo hali iliyopo kwenye mechi nyingi nilizopata kwenda kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Si kwamba mashabiki wa kiume wameamua kuingia kwenye vyoo vya kike kwa makusudi, la hasha.

Ni kwamba vyoo upande wa wanaume vinakuwa vimefungwa. Mazingira ya Uwanja wa Taifa kwa yeyote anayeufahamu ni kwamba upande mmoja ni choo cha wanaume na upande mwingine ni wa wanawake. Kwa sababu asilimia kubwa, yapata 80 ya mashabiki wa soka wanaoingia ni wanaume, basi wanapoona lango la vyoo vya wanaume limefungwa, wanaingia upande wa pili kwa sababu wanaona viko vitupu.

Sijajua ni kwa sababu gani mara nyingi vyoo vya upande wa wanaume huwa vinafungwa kuliko wanawake, lakini hii inaleta usumbufu sana kwenye Uwanja wa Taifa na pia si desturi nzuri si kwa utamaduni wetu, lakini pia kibinadamu.

Uchunguzi wangu mdogo tu nimegundua kuwa unaweza kukuta sehemu moja mlango wa choo cha wanaume kimefungwa na upande wa pili choo cha wanawake kiko wazi, halafu ukizunguka tena sehemu nyingine ya uwanja ndipo utakuta vyoo vya pande zote vinafanya kazi.

Hapa nataka kuwakumbusha tu uongozi wa uwanja unavyotakiwa kufanya. Ni kwamba eneo la mlango wa choo cha wanaume kilichofungwa kwa sababu yoyote ile, wawe wanaweka tangazo la kuwaelekeza wapi waende, kwa sababu baadhi ya mashabiki wakishafika hapo na kukuta mlango umefungwa hawajui kama kuna sehemu nyingine tena kuuzunguka uwanja kuna vyoo vingine.

Hii itawafanya wanaume kuacha kuchukua hatua ya kukimbilia kuingia kwenye vyoo vya wanawake kwa sababu wanaona hakuna tena sehemu nyingine ya kupata haja.

Vile vile inawezekana kabisa kuweka askari kwenye mlango wa kuingilia choo cha wanawake ili kuwazuia wanaume wasiingie na kuwaruhusu wanaotakiwa kuvitumia tu.

Najua vyoo vya wanaume hasa Uwanja wa Taifa vinakuwa na changamoto nyingi kwa sababu baadhi yao hawajatulia, unaweza kukuta wameng'oa koki na kufanya maji yatiririke hadi nje, na uharibufu mwingine mwingi ndiyo maana huenda hali hiyo inajitokeza, lakini uongozi wa uwanja uhakikishe siku za mechi yoyote ile hasa inayopokea mashabiki wengi  vyoo vyote vya wanaume na wanawake vinafanya kazi ili kuepuka adha hiyo kwa mashabiki wanawake.

Kwa sasa mpira wa miguu umepata bahati ya kuanza kupendwa na wanawake na wameshaanza kuwa wanajitokeza kwenda viwanjani, hivyo inabidi wapatiwe huduma zote muhimu zinazohitajika bila kuwabughudhi na kuwaudhi hali inayoweza kusababisha kususa kwenye viwanjani.

Shirikisho la Soka nchini (TFF), linaweza kukaa na uongozi wa Uwanja wa Taifa kuangalia suala hili.