Wachezaji waliorejea nyumbani msimu huu

09Sep 2019
Adam Fungamwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wachezaji waliorejea nyumbani msimu huu

WAKATI raundi ya kwanza ya Ligi Kuu Tanzania Bara imekamilika kwa timu zote 20 kucheza mechi za kwanza, kuna baadhi ya mambo mbalimbali yamejitokeza, huku ikishuhudiwa baadhi ya wachezaji wakizichezea timu zao za zamani baada ya kurejea tena.

Wachezaji hao zamani walikuwa kwenye timu hizo, lakini waliondoka kwa sababu mbalimbali, ikiwamo viwango vyao kushuka, kukosa namba za kudumu au kutafuta maisha, lakini kwa msimu huu wa Ligi Kuu 2019/20 wamerejea tena kwenye timu hizo...

1. Benedict Tinoco- Kagera Sugar

Amerejea tena Kagera Sugar. Ni golikipa wa zamani wa timu hiyo, kabla ya kuihama mwaka 2015 na kujiunga na Yanga.

Alikaa kwenye timu hiyo kwa msimu mmoja, lakini hakuwa na msimu mzuri, kabla ya kutolewa kwa mkopo Mtibwa Sugar.

Huko alikuta kipa mkongwe Shaaban Kado, lakini akapambana hadi kuwa kipa namba moja, akionyesha uwezo wa hali ya juu, mpaka kusababisha timu hiyo kutwaa Kombe la FA na kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2017/18.

Hata msimu uliopita alikuwa kwenye kiwango cha hali ya juu, kiasi cha klabu yake ya zamani Kagera Sugar ikamezea mate na kumrejesha nyumbani msimu huu.

2. Mohamed Said Nduda- Mtibwa Sugar

Msimu huu Nduda ameanza kuichezea klabu yake ya zamani, Mtibwa Sugar. Amerejea nyumbani akitokea kwenye klabu ya Ndanda FC.

Alikuwa kwenye klabu ya Mtibwa Sugar kabla hajasajiliwa na Simba mwaka 2017, lakini alidumu kwa msimu mmoja tu kabla ya klabu hiyo haijamtoa kwa mkopo kwenda Ndanda FC.

Msimu huu amemaliza muda wake wa mkopo na kuwa huru. Akaamua kurejea kwenye klabu yake ya zamani, Mtibwa Sugar.

3. Haruna Shamte- Simba

Shamte amerejea tena kwenye klabu hiyo baada ya miaka mitano. Beki huyo wa kulia, alijiunga na klabu ya Simba mwaka 2008 na kuichezea kwa mafanikio hadi 2014, alipoondoka na kujiunga na klabu ya JKT Ruvu ambayo kwa sasa inajulikana kama JKT Tanzania. Mwaka 2016 aliondoka na kwenda kujiunga na Mbeya City, hadi 2018 alipochukuliwa na Lipuli.

Akacheza kwa mafanikio makubwa msimu mmoja tu, kabla ya Simba kumrejesha tena nyumbani msimu huu.

4. Shaaban Chilunda- Azam

Straika Chilunda naye ni mmoja wa wachezaji waliorejea nyumbani kwenye klabu yake ya Azam FC. Tofauti na wengine ambao walikuwa kwenye klabu za hapa nchini, yeye alikuwa nchini Hispania akicheza soka la kulipwa.

Aliondoka nchini mwaka juzi kwenda kujiunga na CD Tenerife. Hakuwapo kwenye Ligi Kuu msimu uliopita. Hatimaye msimu huu amerejea tena Azam FC, klabu ambayo alijiunga nayo tangu mwaka 2012.

5. Miraji Athumani- Simba

Ni mmoja kati ya vijana waliolelewa na kupandishwa kutoka kwenye kikosi cha pili cha Simba 2013.

Hata hivyo, hakuna mchezaji aliyeweza kupata namba kwenye kikosi cha kwanza, hivyo 2015 winga huyo asilia, anayemudu kucheza pande zote kushoto na kulia akaondoka kwenda kuichezea klabu ya Toto African ya Mwanza.

Mwaka unaofuata akaondoka na kwenda kujiunga na Mwadui FC, kabla ya msimu uliopita kuichezea Lipuli FC.

Alicheza kwa mafanikio makubwa kiasi cha kuwavutia tena Simba, iliyoamua kumsajili na kumrejesha tena nyumbani alikoondoka miaka sita iliyopita.

6. Erick Kyaruzi- Kagera Sugar

Kagera Sugar imemrejesha tena kundini beki wake wa kati, Erick Kyaruzi ambaye msimu uliopita alichezea Mbeya City.

Alijiunga na Mbeya City 2017, baada ya mkataba wake na Kagera Sugar kumalizika. Kabla ya hapo alikuwa amesimamishwa na klabu ya Kagera Sugar kwa madai ya kuihujumu timu hiyo ilipocheza dhidi ya Yanga msimu wa 2016/17 na kufungwa mabao 6-2.

Akiwa Mbeya City alionekana kuwa kwenye kiwango cha hali ya juu kiasi cha waajiri wake wa zamani kusahau yaliyopita na kuamua kumrejesha ili kuanza upya.

7. Dotto Shaaban- Prisons

Prisons imemrejesha tena kiungo wake za zamani Dotto Shaaban baada ya kumshuhudia akitamba na kuwa mmoja wa wachezaji nyota kwenye Ligi ya Mabingwa wa Mkoa wa Dar es Salaam, akiichezea timu ya Magereza Dar.

Mchezaji huyo aliichezea Prisons msimu wa 2017/18, lakini alipata majeraha yaliyomweka msimu mzima nje, na alipopona akaenda kujiunga na Magereza Dar. Uwezo wake aliouonyesha ulimfanya kukumbukwa tena na waajiri wake wa zamani na kumrudisha kumpa nafasi nyingine.

8. Jabir Aziz- JKT Tanzania

Ni kiungo mbunifu mwenye uwezo mkubwa ambaye msimu huu anaichezea JKT Tanzania, timu ambayo alishawahi kuichezea mwaka 2014, wakati huo ikiitwa JKT Ruvu.

Ni mchezaji mkongwe ambaye safari yake ya soka ilianzia klabu ya Ashanti FC 2007, kabla ya kijiunga na Simba 2008 na kuitumikia kwa miaka miwili, 2010 akatimkia Azam FC.

Baada ya hapo ndipo alipojiunga na JKT Ruvu, kabla ya kwenda Mwadui, Ruvu Shooting na Ndanda, lakini msimu uliopita alikuwa akiichezea timu iliyoshuka daraja ya African Lyon na kufanya makubwa kiasi cha JKT Tanzania kuamua kumrejesha nyumbani.

Habari Kubwa