Nyota 7 wanaovaa na kuitendea haki jezi Na. 7

09Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
LONDON, England
Nipashe
Nyota 7 wanaovaa na kuitendea haki jezi Na. 7

KABLA ya msimu wa 2019/20 haujachanganya, hapa tunawaangalia wacheza saba bora wanaovaa jezi namba saba ambao wapo kwenye kiwango bora zaidi. Jezi namba saba imekuwa ikiwaibua nyota wakubwa zaidi wa soka duniani, kuanzia kina David Beckham hadi Cristiano Ronaldo.

Cristiano Ronaldo.

Makala haya yanakuchambulia wachezaji saba bora kwa sasa ambao wanavaa jezi namba saba, shuka nayo...

7. Jose Callejon

Mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid amekuwa na kiwango cha kuvutia pale Napoli na alianza chini ya kocha, Maurizio Sarri na sasa akiwa na kocha mpya, Carlo Ancelotti.

Amekuwa nguzo muhimu tangu ajiunge na Gli Azzurri hao mwaka 2013 na amefunga mabao 79 na kutoa pasi za mwisho 69.

6. Jadon Sancho

Akiwa anacheza katika klabu ya Borussia Dortmund, kinda huyo amekuwa na kiwango cha kuvutia kwani amefunga mabao 15 kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani na kuweka rekodi ya mchezaji kijana zaidi kwenye ligi hiyo kufunga idadi hiyo ya mabao, rekodi ambayo ilidumu kwa kipindi cha miaka 52.

5. N'Golo Kante

Licha ya kuwa anacheza kiungo mkabaji, lakini Kante amekuwa akiitendea haki jezi namba saba. Tangu alipojiunga Chelsea, amekuwa na wakati wa kuvutia zaidi kwa kiwango chake kuendelea kuimarika.

4. Son Heung-min

Tottenham Hotspur mara zote imekuwa haina historia ya kupata mawinga bora. Na wakati Gareth Bale anaondoka hakuna aliyejua kama Spurs itapata winga bora, Son Heung-min raia wa Korea Kusini.

Amekuwa akitendea haki jezi namba saba, huku akifunga mabao 20 na kutoa pasi za mwisho 10 katika mashindano yote msimu uliopita akiichezea Spurs.

3. Raheem Sterling

Manchester City ina moja ya safu bora zaidi ya ushambuliaji kwenye Ligi Kuu ya England na Ulaya. Na mmoja wa wachezaji ambaye anayeunda safu hiyo ya kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola ni Sterling.

Nyota huyo alifunga mabao 17 na kutoa pasi za mwisho 10 kwa msimu wa 2018/19 akicheza mechi 34.

2. Kylian Mbappe

Akiwa na umri wa miaka 20 nyota huyu wa klabu ya Paris Saint-Germain tayari ana mafanikio makubwa kwenye mchezo wa soka. Katika umri wake wachezaji wengi wanakuwa na ndoto ya kushinda mataji makubwa mbeleni.

Lakini tayari Mbappe ana taji la Kombe la Dunia alilolitwaa akiwa na kikosi cha Ufaransa mwaka jana.

Msimu uliopita alifunga mabao 33 na alizidiwa na Lionel Messi katika mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu kwa ufungaji bora Ulaya. Messi alikuwa na mabao 36 akimzidi Mbappe kwa matatu tu.

1. Cristiano Ronaldo

Huyu ndiye unaweza kusema mchezaji bora zaidi kuvaa jezi namba saba duniani. Kwa sasa akiwa na umri wa miaka 34, lakini kiwango chake bado kinaonekana kuwa bora zaidi na hata muda wa kucheza unaonekana kuwa bado kwake.

Akiwa ameanza kucheza soka kule Benfica nchini Ureno, akatua Manchester United akicheza kwa mafanikio makubwa, kabla ya kutimkia Real Madrid ambako nako ameacha alama kubwa kwenye Ligi Kuu ya Hispania.

Akiwa Real Madrid, Ronaldo aliweka rekodi ya kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo kabla ya kuamua kutimkia katika klabu ya Juventus ya nchini Italia ambako anacheza hadi sasa,

Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Ronaldo alisema anataka kucheza hadi afikishe umri wa miaka 40, kwani anaamini ana uwezo huo.

Habari Kubwa