TPDC yakutanisha wadau bomba la mafuta

10Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
TPDC yakutanisha wadau bomba la mafuta

SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), limesema lipo katika majadiliano na washirika wa mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga-Tanzania yatakayowezesha mradi huo kuendelea.

Ujenzi huo ulitarajiwa kukamilika 2020, lakini hivi karibuni moja ya kampuni inayoshiriki kutoa mtaji za Total Oils ya Ufaransa, ilitangaza uwezekano wa kujitoa kwenye mradi huo.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa kwenye moja ya magazeti (siyo Nipashe), TPDC ilisema kuwa majadiliano hayo yatahitimishwa na makubaliano yatakayowezesha mradi kuendelea.

"Katika kipindi chote TPDC imeendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi mkubwa, hivi karibuni kumekuwapo na taarifa za kuchelewesha kwa mpango wa mradi kutokana na washirika kuchukua muda mrefu kukubaliana na masuala ya fedha," ilisema taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji.

Kwa mujibu wa TPDC, washirika bado wana nia ya dhati ya kuendelea na utekelezaji wa mradi huo kwa kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Tanzania na Uganda kuona mradi unakamilika kwa ufanisi.

Vile vile, TPDC iliuhakikishia kwamba changamoto za namna hiyo kwenye miradi mikubwa ya kisekta na kimkakati ni ya kawaida.

Uzinduzi wa mradi huo ulifanywa na marais wa nchi za Uganda na Tanzania mwaka 2017 baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,120, ambalo litaweza kutoa ajira zaidi za ya 15,000.

Septemba 6, wakati wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uganda, Rais John Magufuli, alieleza kukerwa na ucheleweshaji wa mradi huo unaofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali ya Uganda, huku akimshauri Rais wa Uganda, kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Ujenzi wa bomba hilo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Dola za Marekani Sh. bilioni nne na tayari Serikali ya Tanzania ilishaanza kulipa fidia kwa wananchi wa vijiji vitakavyopitiwa na mradi huo.

Shughuli zitakazotoa ajira ni ujenzi wa tangi za mafuta, usafirishaji, mawakala mbalimbali wa mafuta watakaokuwapo mkoani Tanga na Uganda.

Habari Kubwa