Wakulima wazidi kulilia mfumo stakabadhi ghalani

10Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
MOROGORO
Nipashe
Wakulima wazidi kulilia mfumo stakabadhi ghalani

MUUNGANO wa vikundi vya wakulima nchini (MVIWATA), umelalamikia uamuzi wa kusitishwa kwa shughuli za ushirika, ukisema hatua hiyo ni sawa na kuisaliti ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Veronika Sophu.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Veronika Sophu, alipoongea na Nipashe kuhusu hali ya sekta ya kilimo nchini na changamoto zinazowakabili wakulima, mjini Morogoro.

Alisema MVIWATA imesikitishwa na hatua kusitisha mfumo wa ushirika (stakabadhi ghalani) kwa mazao ya dengu, choroko, soya, ufuta na mbaazi.

Sophu alisema, mazingira ndani ya Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2010 ibara ya 22 (g) na (w), ziliwekwa mahususi kwa ajili ya kuuinua mfumo wa ushirika na kumsaidia mkulima.

“Sasa haiwezekani mambo yaliyopigiwa debe na wakubwa serikalini, yanakuja kusitishwa kwa utashi wa watu wachache, hilo sio jambo la kulikalia kimya hata kidogo,” alisema Sophu.

Alisema uamuzi uliofanywa dhidi ya mfumo huo haukubaliki na kumwomba Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, kuwafikishia wakulima kilio chao kwa Rais John Magufuli.

Mfumo huo ulisitishwa rasmi Septemba 3, mwaka huu.

Habari Kubwa