Wataka kutengewa maeneo ya kilimo

10Sep 2019
Grace Mwakalinga
mbarali
Nipashe
Wataka kutengewa maeneo ya kilimo

WAKULIMA wa parachichi katika Kijiji cha Lunwa, Mbarali mkoani Mbeya, wameishauri serikali kutenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana ili waongeze uzalishaji wa zao hilo na kujikwamua kiuchumi.

Ushauri huo waliutoa mwishoni mwa wiki wakati wakipata elimu ya namna bora ya kulima na kuzalisha zao hilo kwa tija na kuendana na teknolojia iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) kituo cha Uyole.

Mmoja wa wakulima hao, Jacqueline  Moses,  alisema lengo la serikali ni kuhakikisha nchi inafikia uchumi wa kati, hivyo lazima yatengwe maeneo rasmi kwa ajili ya vijana kufanya shughuli za kilimo.

Alisema kwa sasa kuna kundi kubwa la vijana wasio na ajira, hivyo sehemu pekee itakayowawezesha kujikwamua na umaskini ni kujiingiza kwenye kilimo hususani cha maparachichi ambacho kinafaida kubwa.

"Vijana wengi wako mtaani hawana ajira au shughuli maalum ya kufanya. Kilimo ndiyo ajira ya uhakika iliyobaki lakini changamoto iliyopo ni uhaba wa maeneo ya kufanyia shughuli hiyo. Tunaomba serikali itenge maeneo rasmi kwa vijana ili wajiingize kwenye kilimo cha parachichi," alisema.

Moses alisema licha ya kuwapo changamoto ya ardhi, aliwashauri vijana kutobweteka badala yake watumie fursa zinazopatikana hususan kilimo cha parachichi na kulima kibiashara.

Aliongeza kuwa mradi wa kuhamasisha kilimo cha parachichi utawasaidia kujikwamua kiuchumi na kutoa ajira kwa vijana na kuahidi kufuata maelekezo wanayopewa na wataalamu wa kilimo.

Ofisa Ugani Kata ya Igurusi, Pius John, alisema mradi wa parachichi utarahisisha upatikanaji wa mbegu ukilinganisha na ilivyokuwa awali wakulima kufuata mbegu hizo kwenye vituo vya utafiti, huku akiongeza kuwa uelewa mdogo wa wakulima juu ya kilimo ni changamoto.

Mtafiti wa Matunda kutoka Tari- Uyole, Daud Mbongo, alisema wakulima wajikite katika kilimo cha parachichi kwa sababu ni zao linalolipa kwa sasa.

Alisema mradi wa parachichi katika kijiji hicho utakuwa na tija kwa wakulima hao kwa kuwa watazalisha kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa na kusisitiza kuwa taasisi hiyo itaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.

Habari Kubwa