Mil. 500/- zichochee ujenzi wa hospitali

10Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mil. 500/- zichochee ujenzi wa hospitali

KATIKA toleo letu la leo tumechapisha habari ikieleza kuwa ujenzi wa hospitali za wilaya 67 zinazoendelea kujengwa, umeongezewa nguvu, baada ya  Rais John Magufuli kutoa fedha za ziada kwa ajili ya kuzikamilisha.

Katika kuchochea na kuharakisha ujenzi huo, Rais Magufuli ametoa Sh. milioni 500 kwa kila hospitali hizo mpya za wilaya zinazoendelea kujengwa nchini ili kujenga wodi za kulaza wagonjwa.

Hayo yalibainishwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chamwino inayojengwa kijiji cha Mlowa Barabarani mkoani Dodoma.

Jafo alisema jumla ya Sh. bilioni 33.5 zinatarajia kutolewa kwa ajili ya kujenga wodi katika hospitali hizo mpya za wilaya zinaoendelea kujengwa ambapo kila mmoja itapewa Sh. milioni 500.

Kwa mujibu wa Waziri  Jafo, baada ya kukamilika kwa majengo saba yaliyojengwa katika awamu ya kwanza, Rais Magufuli ametoa kiasi hicho cha fedha zinakazotumika kujenga wodi za kulaza wagonjwa.

Hata hivyo, alisema fedha hizo hazitatolewa hadi zile za awali za ujenzi wa majengo saba ambazo zilitolewa Sh. bilioni 1.5 kwa kila hospitali, majengo yake yakamilike kwa asilimia 100.

Utoaji wa fedha hizo kwa ajili ya kujenga wodi za wagonjwa ni hatua nzuri na muhimu katika suala zima la uboreshaji wa sekta ya afya  nchini. Umuhimu huo unatokana na sababu kuwa haiwezekani hospitali ikajengwa na kuonekana imekamilika bila kuwa na wodi za kulaza wagonjwa.

Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kuwa ili kuwa na hadhi ya kuitwa hospitali, lazima mambo ya msingi yakamilishwe ikiwamo wodi za kulaza wagonjwa, maabara, vifaa tiba na dawa pamoja na miundombinu nyingine.

Kutolewa kwa kiasi hicho kikubwa cha fedha, tunaamini kuwa kutachochea kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hizo ambazo zina umuhimu na tegemezi kwa wananchi wengi katika ngazi ya wilaya.

Tunasema hivyo kutokana na wananchi wengi kuzitegemea zaidi hospitali za wilaya kwa huduma kubwa za matibabu ambazo haziwezi kupatikana katika zahanati na vituo vya afya ngazi ya vijiji na kata.

Sekta nyingine muhimu za jamii pia zina mahitaji makubwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi, hivyo Rais Magufuli amefanya hivyo kwa kuthamini umuhimu wa sekta ya afya.

Kutokana na hilo, kuna kila sababu kwa wahusika na wenye dhamana kuhakikisha kwamba wanazifuatilia na kuzisimamia fedha hizo ili zitumike kwa lengo lililokusudiwa la kukamilisha ujenzi wa hospitali hizo 67 za wilaya.

Kumekuwapo na matukio ya ufujaji, wizi na ubadhirifu wa fedha za miradi kadhaa ya jamii nchini  ikiwamo ya sekta ya afya, hivyo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wakuu wa mikoa husika watatimiza wajibu wao kwa kuhakikisha kuwa hakuna hata senti moja itakayochakachuliwa katika ujenzi wa hospitali hizo. Kwa watakaodiriki kuzichakachua wasionewe aibu badala yake wakamatwe na kushtakiwa kwa makosa ya kuhujumu uchumi.

Ni matarajio yetu kwamba fedha zilizotolewa na Rais Magufuli zitasaidia kuchochea ujenzi wa hospitali hizo ili zitoe huduma za afya kwa wananchi wengi.

Habari Kubwa