Serikali isimamie maagizo yake magari ya wanafunzi

10Sep 2019
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
Serikali isimamie maagizo yake magari ya wanafunzi

KWA muda sasa, serikali iliagiza magari yote yanayobeba wanafunzi yapakwe rangi ya njano ili kutambulisha na kuwezesha wanafunzi kusafiri kwa urahisi.

Utekelezaji wa jambo hilo ulianza baada ya kutokea ajali ya wanafunzi 32 wa Luck Vicent mkoani Arusha, waliofariki baada ya gari lao kupata ajali wakielekea Manyara, kufanya mtihani wa kujipima.

Toka wakati huo, serikali ilielekeza magari ya wanafunzi kupakwa rangi ya njano kwa mujibu wa sheria.

Hiyo ilitokana na wengi kutumia magari ya kawaida kama ‘Noah’ na daladala ambazo hukodishwa kwa muda mfupi kubeba wanafunzi.

Magari hayo ya kukodishwa huendeshwa na madereva wasio na utaalamu wa kuendesha wanafunzi, jambo ambalo kimsingi ni la hatari.

Baada ya maelekezo hayo mabadiliko yalitokea kwa magari kupakwa rangi na hivyo kutambulika kirahisi kuwa ni ya kubeba wanafunzi.

Hata hivyo, bado kuna magari ya kawaida yanayotumiwa kubeba wanafunzi kwa baadhi ya shule.

Hivi sasa shule zimefungwa kwa wiki mbili, matarajio ni kufanya marekebisho mbalimbali kwenye shule, ikiwamo kuhakikisha kunakuwa na magari na madereva waliofundishwa namna ya kuendesha magari ya wanafunzi.

Ni vyema serikali ikafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maagizo yake likiwamo la shule kuwa na magari yake ya kubeba wanafunzi, kuliko kila shule kujiamulia itakavyo.

Kuna changamoto kubwa ya wanafunzi kubanana kupita kiasi katika baadhi ya magari, kutokana na uhaba wa magari hayo kwa baadhi ya shule licha ya wazazi kulipa viwango vikubwa vya ada, ambavyo huongezwa kila wakati.

Wazazi hukubaliana na ongezeko la fedha za usafiri au ada kwenye shule binafsi kwa sababu wanataka watoto wao wapate kilicho bora, ikiwamo kusafiri vizuri na kufikishwa shuleni kwa wakati.

Tofauti na matarajio ya wazazi, shule huwa na malengo ya kufanya biashara, na ndiyo mwanzo wa wanafunzi kujazwa kwenye mabasi au ‘Noah.’

Tatizo jingine ni ubovu wa magari hayo kwani kwa shule ambazo zimejitahidi kuwa na magari yao, mengine ni yaliyokuwa yanatumika kwenye usafiri wa umma na sasa yamegeuzwa kubeba wanafunzi.

Matokeo yake huharibika mara kwa mara na kusababisha wanafunzi kuteseka njiani.

Kutokana na adha hiyo wanafunzi wanachelewa kuchukuliwa vituoni, kufika shuleni na kurudishwa nyumbani.

Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na shule binafsi lakini eneo la usafirishaji limesahaulika na ambalo ni muhimu sana kwa maslahi ya wanafunzi.

Ni vyema shule zikajipanga kuhakikisha suala la usafiri halina ubabaishaji. Serikali ifanye ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuondoa usumbufu kwa wazazi na wanafunzi.

Kasi ya kutoa maelekezo na kufuatilia ajali inapotokea inapaswa kwenda sambamba na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo hayo, kwamba magari yote yanayobeba wanafunzi yamepakwa rangi ya njano na kutambulisha kisheria na yanakaguliwa mara kwa mara.

Ukaguzi wa mara kwa mara utaondoa usumbufu au uwezekano wa kutokea ajali, kwani kutakuwa na magari sahihi ya kusafirishia wanafunzi na siyo kuwa na magari yenye uhakika wa kuondoka lakini hakuna uhakika wa kufika.

Aidha, ni muhimu kukawa na marufuku kwa ya magari mengine kutumika kubeba wanafunzi, kwa sababu madereva wa kubeba wanafunzi wanapaswa kuwa na maadili na waliofundishwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Kutumia magari ya daladala mathalani si jambo jema kwa sababu ya lugha isyo ya staha inayotumiwa na madereva ama makondakta wao lakini aina ya muziki unaopigwa pia kwenye magari hayo unawafanya wanafunzi wadogo kuigiza mambo yasiyo sahihi kwa umri wao.

Ikiwa gari asubuhi na jioni linapiga nyimbo ambazo pengine zimekataliwa na serikali, upo uwezekano wa wanafunzi kukariri hilo.

Hata hivyo, kwa madereva na makondakta waliofunzwa maalumu kwa kazi hiyo hawawezi kuweka nyimbo hizo au kutumia lugha mbaya.