Yanga yasaidiwa  kuimaliza Zesco

10Sep 2019
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga yasaidiwa  kuimaliza Zesco
  • ***Yathibitisha kupokea taarifa kutoka Bodi ya Ligi Kuu kuhusu mabadiliko waliyofanya ili kuhakikisha...

YANGA imerahisishiwa njia ya kuhakikisha inasonga mbele kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Bodi ya Ligi Kuu kusogeza mbele mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City ili kuwapa nafasi wawakilishi hao wa Tanzania kujiandaa vema na mechi yao ya raundi ya kwanza dhidi ya Zesco ya Zambia.

Ratiba ya awali ilikuwa ikionyesha baada ya mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kati ya Yanga na Zesco Jumamosi Septemba 14, kikosi hicho kinachonolewa na Mwinyi Zahera, kingecheza mchezo mmoja wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City kabla ya kwenda kurudiana na Zesco ugenini Septemba 22.

Hata hivyo, Bodi ya Ligi Kuu kupitia kwa Mtendaji wake Mkuu, Boniface Wambura, imeuondoa mchezo huo dhidi ya Mbeya City na sasa utapangiwa tarehe nyingine, hivyo kutoa mwanya kwa Yanga kujiandaa vema kabla ya kurudiana na Zesco.

Tayari Bodi ya Ligi Kuu imewaandikia Yanga na Mbeya City barua kuwajulisha mabadiliko hayo ambapo Yanga kupitia kwa mratibu wake, Hafidh Saleh imethibitisha kuipata.

"Ni kweli mchezo na Mbeya City haupo tena na hii kwetu ni faraja kuona tutakuwa na muda mzuri kujiandaa na mchezo wetu wa marudiano ugenini," alisema Saleh.

Endapo Yanga itawatupa nje Zesco itatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, kama itaong'olewa na Wazambia hao itaangukia kucheza mechi ya mchujo na mojawapo ya timu zitakazofuzu raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika kusaka nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya shirikisho.

Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Township Rollers ya Botswana kwa jumla ya mabao 2-1 ikitoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kabla ya kushinda ugenini 1-0.

Timu nyingine ya Tanzania inayoshiriki michuano ya CAF ni Azam FC, ambayo Ijumaa itaikaribisha Triangle FC ya Zimbabwe kwenye Kombe la Shirikisho.

Azam imetinga hatua hiyo baada ya kuitoa Fasil Kenema ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 3-2.

Habari Kubwa