Kaseja atoa siri ya penalti miaka 19

10Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kaseja atoa siri ya penalti miaka 19

BAADA ya kuibeba Tanzania kwa kuiongoza Taifa Stars kuitoa timu ya Taifa ya Burundi kwenye mechi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia nchini Qatar 2022, kipa mkongwe nchini, Juma Kaseja, ametoa siri ya miaka 19 ya uhodari wake wa kucheza penalti.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Taifa na Stars kusonga mbele kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 3-0 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Kaseja aliendeleza ubora wake wa kucheza penalti kwa mara ya pili mfululizo tangu arejeshwe Stars, ikiwa ni baada ya mwezi uliopita kucheza tena penalti wakati wakiitoa timu ya Taifa ya Kenya, Harambee Stars kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani, CHAN.

Akizungumza baada ya mechi hiyo juzi, Kaseja alisema uwezo wake wa kucheza mikwaju ya penalti hajafundishwa na kocha yeyote na kwamba hicho ni kipaji chake na kujituma kwake.

"Katika kipindi cha miaka 19 nilichocheza soka kuanzia ngazi ya chini hadi Ligi Kuu sijawahi kufundishwa na mtu yeyote namna ya kudaka penalti, hiki ni kipaji changu kutoka kwa Mungu," alisema Kaseja.

Kaseja ambaye alishaporwa namba katika kikosi cha Taifa Stars na Aishi Manula wa Simba kabla ya Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Etienne Ndayiragije kumrejesha akianza na mechi hiyo ya CHAN dhidi ya Harambee Stars, mbali na kucheza penalti hizo alionyesha uwezo mkubwa kwa kuokoa hatari kadhaa kabla ya hatua hiyo ya penalti.

Katika mechi hiyo, Kaseja alianza kwa kuidaka penalti ya Omari Ngando, kisha Saedo Berahino na Gael Bigirimana walikosa penalti zao kwa kupiga nje huku zile za Taifa Stars zikizamishwa kimyani na Erasto Nyoni, Himid Mao na Gadiel Michael.

Kwa matokeo hayo, Taifa Stars ambayo inasubiri kukutana na Sudan kwenye mechi ya raundi inayofuata ya kuwania kufuzu CHAN, pia sasa inasubiri ratiba ya makundi kutoka Shirikisho la Soka Afrika (Caf), kujua timu watakazopangwa kundi moja kuwania kufuzu Kombe la Dunia Qatar 2022.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Taifa Stars ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, jana alimkabidhi Kaseja Sh. milioni 10 kwa kuwa nyota wake wa mchezo wa juzi dhidi ya Burundi, hiyo ikiwa ni ahadi aliyokuwa ameitoa.

Habari Kubwa