Simba, Mtibwa Sugar sasa zawaishwa Uhuru

10Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Simba, Mtibwa Sugar sasa zawaishwa Uhuru

WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wakiendelea kujifua katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, Bodi ya Ligi Kuu imerudisha nyuma mechi yao ya ligi hiyo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Awali mechi hiyo ilikuwa ipigwe Septemba 18, mwaka huu katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, lakini sasa mchezo huo utapigwa Ijumaa Septemba 13, wiki hii katika dimba hilo maarufu 'Shamba la Bibi'.

"Mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao ulipangwa kuchezwa Septemba 18, mwaka huu umerudishwa nyuma na sasa utachezwa Ijumaa Septemba 13, saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam," ilieleza taarifa ya Simba.

Nipashe lilipomuuliza Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Cliford Ndimbo, sababu za  mabadiliko hayo ya ratiba kwa mechi hiyo ya Simba, alisema yametokana na timu hiyo kutolewa kwenye mashindano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo sasa kutokukabiliwa na ratiba ngumu.

"Awali ratiba hiyo ilipangwa ikilenga kwamba Simba ingeweza kuendelea na michuano ya kimataifa, lakini sasa imetolewa hivyo inaweza kucheza kwa sababu haikabiliwa na ratiba ngumu ndiyo maana kumefanyika mabadiliko hayo," Ndimbo alisema.

Simba iliyokuwa ikiiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilitolewa raundi ya awali na UD Songo ya Msumbiji kwa faida ya bao la ugenini baada ya kulazimisha suluhu nchini humo kabla ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine uongozi wa Mtibwa Sugar umeshaweka wazi lengo la kupata pointi tatu za kwanza msimu huu baada ya kukubali kupoteza katika mechi ya ufunguzi kwa kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Lipuli FC kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.

“Tulipoteza mbele ya Lipuli sasa ni muhimu kwetu kushinda mchezo wetu dhidi ya Simba, tunahitaji kupata pointi tatu zao ili kujiweka kwenye mazingira ya ushindani," Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru alisema.

Habari Kubwa